GAMBOSHI ASKOFU AKUTANA NA WAGANGA WA KIENYEJI

 

 



ASKOFU wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu amekutana na Waganga wa tiba asili na tiba mbadala katika kijiji cha Gamboshi wilayani Bariadi Mkoani Simiyu kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali ikiwemo kuhamasisha maendeleo, imani, pamoja na kuenzi mila na desturi za kabila la Wasukuma.

Askofu Sangu ameyasema hayo jana Oktoba 19, 2021 katika eneo la Kigango cha Gamboshi ambapo amewataka waganga kulinda mila na desturi za kabila la wasukuma, kupiga vita ndoa za jinsia moja, utoaji mimba pamoja na mauaji ya watu wenye ulemavu.

Katika hotuba yake Askofu Sangu amewataka waganga hao kuwa sehemu ya kulinda tamaduni za kabila la wasukuma ili jamii iepukane na masuala ya utoaji mimba na ndoa za jinsia moja ambazo zinadhalilisha utu wa mtu na kwamba waganga hao wanatibu watu kwa asilimia kubwa sana.

“Mila na desturi mtazilinda ninyi, kuna mengi yanafanyika katika jamii yetu…kupitia nafasi ,mlizonazo katika jamii, tukapandikize uhai katika maisha ya binadamu, tulinde uhai wa binadamu tangu mimba inapotungwa hadi mtoto anapozaliwa”, amesema Askofu Sangu.

Hata hivyo amesema huko nyuma (zamani) watu wenye ulemavu wa ngozi walikuwa wakiuwawa bila hatia na kwamba lawama zote walitupiliwa waganga wa kienyeji jambo ambalo lilikuwa linaleta ukakasi katika jamii na kuonekana waganga hao hawana tija katika jamii.

No comments:

Post a Comment