Wataalam wa Umoja wa Mataifa Jumatatu ya wiki hii walielezea wasiwasi wao mkubwa kufuatia tuhuma nyingi za unyanyasaji wa kijinsia unaofanywa dhidi ya watoto katika taasisi za Kanisa katoliki na kuitaka makao makuu ya Kanisa katoliki Vatican kufanya juhudi zaidi kuzuia ghasia na unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto.
Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja huo wa mataifa imeripoti kuwa wataalamu hao wameutoa wito huo kutokana na kwamba makao makuu ya kanisa katoliki Vtaican, haitoi ushirikiano wowote katika kuchunguza madai ya kufanyika unyanyasaji wa kiongono dhidi ya watoto.
Wataalamu hao wameeleza kuwa kuna udanganyifu mkubwa unaofanyika katika juhudi za kanisa za kutaka kuficha ukweli, na pia kuwalinda wahusika wa vitendo hivyo, lakini pia kukwepa kulipa fidia wanazopaswa kupewa waathiriwa wa vitendo hivyo.
Katika Barua yao ya tarehe 7 Aprili mwaka huu ambayo ilitangazwa kwa umma Jumatatu wiki hii, wataalamu hao pia wamesema kuwa unyanyasaji huo ulitekelezwa zaidi ya miongo kadhaa iliyopita katika nchi nyingi huku kukiwa na maelfu ya waathiriwa ambao wamenyamazishwa.
Umoja wa mataifa umesema baadhi ya wajumbe wa kanisa hilo miongoni mwao maaskofu na mapadri wamekuwa wakizuia utekelezwaji wa sheria za nchi za wahusika wa makosa ya unyanyasajii wa kingono wa watoto.
Hata hivyo makao makuu ya Vatican haijatoa tamko lake kwa umma kujibu barua.
No comments:
Post a Comment