MCHUNGAJI wa Kanisa la Maombezi jijini Dar es Salaam (GRC), Antony Lusekelo ameukosoa waraka wa Baraza la Maaskofu Katokili Tanzania (TEC) na kudai kuwa waraka huo unachochea mgawanyiko na kuleta mtafaruku wa amani ndani ya nchi.
Amesema waraka huo ambao umeshasomwa katika makanisani yote ya kikatoliki nchini, haukutolewa katika muda sahihi hasa ikizingatiwa nchi ipo katika mtikisiko unaotokana na mjadala wa uwekezaji kwenye badandari ya Dar es Salaam.
Mchungaji Lusekelo ametoa kauli hiyo Agosti 22, 2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Ubungo Kibangu jijini Dar es salaam.
Akiuchambua waraka huo, mbali na kusisitiza kuwa anauheshimu sana ukatoliki kwani ndio uliomlea na hata sasa ndio unaoongoza katika ukristo, amesema TEC wametumia vibaya madaraka yao kwani hawakusoma alama za nyakati.
“Ninawataka na kuwashauri TEC wauondoe huo waraka huo, najua upo lakini waunyamazie kimya wasiendelee kuuzungumzia,” amesema Lusekelo.
Aidha, amesema anaunga mkono uwekezaji nchini lakini kuhusu suala hilo la uwekezaji bandarini anaungana na wale wanaotaka hekima na busara itumike kushughulikia kasoro zinazoonekana kwenye mkataba huo wa ushirikiano kati ya Tanzania na Dubai.
Ameongeza kuwa jambo ambalo TEC wangepaswa kufanya ni kuzungumza na viongozi wa serikali kwa kuwa wana uwezo huo na kuwaonesha viongozi hao kasoro waliloziona kisha waje kwenye umma wa Watanzania na kuishauri Serikali kwa hekima kama walivyofanya viongozi wengine badala ya kuukataa uwekezaji huo moja kwa moja kwani hali hiyo imezidi taharuki ndani ya jamii.
“Kutokana na hali hii nawaombea dua maaskofu wote Mwenyezi Mungu awasamehe kwa kuandika waraka huu.” amesema Lusekelo.
Hata hivyo, Mchungaji amesema waraka huo haujaungwa mkono na watanzania au wakatoliki wote ila ni baadhi ya hao maaskofu hao hivyo, wasingepaswa kutumia hoja kudai kuwa watanzania wengi hawaungi mkono.
Tarehe 18 Agosti 2023, TEC ilitoa waraka maalumu uliopinga mkataba huo wa uwekezaji kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai na kubainisha wazi baadhi ya vifungu ambavyo vinaukosesha hadhi ya kuungwa mkono na viongozi hao.
No comments:
Post a Comment