Moshi
Katika Kanisa la CCT Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Askofu Alex Malasusa amesema Pasaka ya 2021 ni ya majonzi, “Pasaka ya mwaka 2021 kwetu Watanzania ni ya pekee sana, kwamba inatukuta katika kipindi cha majonzi, kipindi cha utulivu katika nchi yetu baada ya kifo cha mpendwa wetu Magufuli.”
“Tunamshukuru Mungu kwa maisha yake na ushuhuda wake na hasa kuhimiza kumtegemea Mungu.”
Amebainisha kuwa Watanzania na dunia kwa ujumla kuna la kujifunza kutokana na maisha ya Magufuli, “uongozi wa Magufuli ulikuwa wa pekee nasi kama Tanzania tuna cha kujifunza. Magufuli alikuwa miongoni mwa viongozi wachache kati ya wanasiasa wengi barani Afrika.”
“Alikuwa fahari ya Waafrika na kwa muda mfupi amefanya vitu ambavyo vinahitajika. Afrika inahitaji uongozi, hatuhitaji siasa. Maneno yamekuwa mengi lakini uongozi haupo.”
Askofu Malasusa alimshukuru Rais Samia kwa kupokea kazi ya urais na kuwapongeza Watanzania kwa kuwa na utulivu.
“Mahali pengine siyo kitu kinachojitokeza hivi, Mungu amekuwa juu yetu. Hata wasiotupenda nina uhakika wanapokuwa peke yao wanasema tumekomaa. Sisi tunaendelea kumwombea Rais wetu Samia amweke. Uongozi siyo mtu bali Mungu anayemweka huyo mtu,” amesema.
Mkoani Kilimanjaro mkuu wa KKKT, Akofu Fredrick Shoo amewataka Watanzania kuachana na mtazamo potofu kuhusu uwezo wa wanawake, akisema Mungu atamtumia Samia kuleta matumaini mapya.
Dk Shoo ambaye pia ni Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini ya kanisa hilo aliyasema hayo wakati akitoa salamu za Pasaka, kusisitiza kuwa Mungu atamtumia Samia kama alivyowafanya wanawake kuwa wa kwanza kupata habari za kufufuka kwa Yesu Kristo.
"Niwakumbushe habari hii kuwa Mungu kwa makusudi aliwatumia wanawake wale wakaleta habari za kufufuka kwa Yesu Kristo na wakatangaza habari njema, ndivyo atakavyomtumia Rais wetu Samia kuleta habari njema na matumaini mapya kwa Watanzania.”
"Kama Mungu alivyowatumia wale wanawake walioshuhudia habari za kufufuka kwa Yesu na kuwa wa kwanza kupeleka habari kwa wanafunzi, naamini na Mungu atamtumia vyema mama huyu na ataleta matumaini mapya kwa Watanzania,” amesema.
Amesema katika sikukuu ya Pasaka, Wakristo wanakumbushwa mambo manne ambayo ni upendo wa Mungu, msamaha wa dhambi, matumaini ya uhai mpya na maisha mapya ndani ya Kristo.
Imeandikwa na Elias Msuya, Peter Saramba, Florah Temba, Pamela Chilongola.
No comments:
Post a Comment