Kadinali Laurent Monsengwo, aliyekuwa mkosoaji wa utawala wa Rais wa
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Joseph Kabila amejiuzulu ikiwa ni wiki
chache kabla ya nchi hiyo kufanya uchaguzi mkuu.
Monsengwo mwenye umri wa miaka 79, ambaye pia alikuwa Askofu Mkuu wa
Kanisa Katoliki la Kinshasa, amemuachia Fridolin Ambongo nafasi hiyo.
“Papa Francis leo ameridhia ombi la Kadinali Laurent Monsengwo.
Fridolin Ambongo atachukua nafasi yake,” msemaji wa kanisa hilo la
Kinshasa, Bruno Lusongakio amekaririwa na AFP.
Ukosoaji wa wazi na ukali wa Monsengwo dhidi ya utawala wa Rais
Kabila uliodumu kwa zaidi miaka mingi, unahusisha pia mauaji ya
waandamanaji.
Mwanzon mwa mwaka huu, Kadinali huyo alijihusisha na uratibu wa
maandamano ya kupinga hatua za Rais Kabila kuvuka ukomo wa muhula wa
urais uliwekwa kwenye Katiba. Maandamano hayo yalifanyika siku moja
kabla ya sherehe za siku ya Mwaka Mpya.
Muda wa Rais Kabila kukaa madarakani kwa mujbu wa katiba ulipaswa kukoma
mwaka 2016, lakini aliendelea kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kuweka
sawa hali ya kiusalama wa nchi kabla ya kuitisha uchaguzi.
Hatua hiyo ilipingwa vikali na vyama vya upinzani pamoja na viongozi wa
dini ambao kwa nyakati tofauti waliitisha maandamano. Taifa
hilo litafanya uchaguzi wa kidemokrasia kumpata mrithi wa Rais Kabila
Disemba 23.
No comments:
Post a Comment