Polisi Mkoa wa Kinondoni wanamshikilia
mfanyakazi wa ubalozi wa Syria nchini kwa tuhuma za kumjeruhi usoni
mhasibu wa ubalozi huo, Hassan Alfaouri na kumpora Euro 93,000
(Sh237milioni).
Akizungumza leo Jumatano Machi 21, 2018
kamanda wa polisi mkoani humo, Jumanne Muliro amesema tukio hilo
lilitokea Machi 19, 2018 saa nane mchana eneo la Shule ya Msingi
Oysterbay, jijini Dar es Salaam.
Amesema siku hiyo, mhasibu huyo akiwa
katika gari na dereva wake wakielekea Benki ya Azania tawi la Mazdu
House lililopo mtaa wa Samora wakipeleka fedha hizo, walipofika mtaa wa
Zambia dereva huyo alianza kuendesha gari taratibu.
Amesema baada ya kupunguza mwendo,
alisimama na kuzima gari ghafla walitokea watu watatu; mmoja kati yao
alikuwa na kipande cha nondo mkononi na kuingia katika gari hilo na
kumtaka mhasibu huyo awape fedha.
Muliro amebainisha kuwa uchunguzi wa
awali unaonyesha kuwa tukio hilo lilipangwa na baadhi ya wafanyakazi wa
ubalozi wasio waaminifu, akiwamo dereva huyo ambaye wakati uporaji
ukiendelea, hakutoa msaada wowote.
"Walivyoona anakawia kutoa fedha
walimjeruhi usoni kwa kipande cha nondo, walimshusha dereva kwa nguvu na
kuondoka na gari hilo,” amesema.
Amesema baada ya tukio hilo, polisi walianza msako na kuikuta gari hiyo ikiwa imetelekezwa Msasani Bonde la Mpunga.
No comments:
Post a Comment