Jumla ya sampuli 72,000 zimepimwa na Wakala wa Mkemia Mkuu wa Serikali
(GCLA) katika kipindi cha Januari hadi Desemba, mwaka huu na kati ya
hizo, 1,177 zilikuwa za vinasaba (DNA) ili kutambua uhalali wa wazazi
kwa mtoto na majibu yalibainisha kuwa baba wengi hawakuwa halali.
Akizungumza na Mtanzania Jumapili ofisini kwake juzi, Mkemia Mkuu wa
Serikali, Profesa Samwel Manyele, alisema idadi ya sampuli hizo za DNA
zimepatikana katika majalada 338 yaliyowasilishwa katika kipindi cha
Januari hadi Desemba, mwaka huu yaliyokuwa na lengo la kufanya utambuzi
wa uhalali wa baba kwa mtoto, kesi za jinai, mirathi na utambuzi wa
jinsi tawala za mtoto.
“Katika upimaji wa sampuli za kutambua uhalali wa baba kwa mtoto kwa
mwaka huu, baba wengi walikutwa si wazazi halali wa watoto waliokuwa
wanalalamikiwa,” alisema.
Profesa Manyele alisema idadi ya sampuli hizo kwa mwaka huu zimeongezeka
ukilinganisha na mwaka jana ambazo zilikuwa 554 kati ya majalada 332.
Chanzo- Mtanzania Jumapili
No comments:
Post a Comment