Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa siku
tatu kwa wafanyabiashara na wenye viwanda vya mafuta ya kupikia na
sukari nchini kuhakikisha bidhaa hizo zinaendelea kupatikana katika
maeneo yote na kwa bei ya kawaida.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo jioni
Mei 9, 2018 Bungeni Jijini Dodoma mara baada ya Waziri wa Viwanda,
Biashara na Uwekezaji, Bw. Charles Mwijage kutoa kauli ya Serikali
kuhusu uhaba wa mafuta ya kupikia nchini.
"Natoa siku tatu kuanzia kesho Alhamisi,
Ijumaa na Jumamosi mafuta yote yaliyoko bohari yaondolewe yaendelee
kusambazwa kama kawaida nchini kote ili kuondoa uhaba uliojitokeza na
kamwe Serikali haitokubali kuchezewa na wafanyabiashara wasiowaaminifu",
amesema Majaliwa.
Pamoja na hayo, Waziri Mkuu ameendelea
kwa kusema "kama uhaba wa bidhaa hiyo utaendelea, ifikapo Jumapili
serikali itaanza kufanya msako kwenye viwanda na maghala na kuchukua
hatua kali kwa watakaobainika kuficha mafuta hayo".
Waziri Mkuu amesema takwimu
zinathibitisha kwamba mafuta ya kupikia yaliyoingizwa nchini yanatosha,
hivyo nchi haipaswi kuwa na uhaba.
"Hatuwezi kukubaliana na jambo hili kwa
sababu haliko kwa bahati mbaya ni mpango uliopangwa kwani imekuwa ni
kawaida kila tunapoelekea kwenye Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kunakuwa na
upungufu wa bidhaa hasa sukari, hivyo Serikali haitakubali wananchi
wateseke bila sababu za msingi," amesisitiza.
Akiwasilisha kauli ya serikali Bungeni,
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Mwijage amesema vyanzo
vinavyotumika kuzalishia mafuta nchini vinatosheleza mahitaji kwa
asilimia 30, hivyo asilimia 70 ya mafuta huagizwa kutoka nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment