Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Augustine
Mahiga atafanya ziara ya kikazi nchini Jamhuri ya Watu wa China kuanzia tarehe 17
hadi 21 Desemba 2017 kufuatia mwaliko wa mwenyeji wake, Waziri wa Mambo ya Nje
wa nchi hiyo, Mhe. Wang Yi.
Balozi Mahiga anayetarajiwa kuondoka nchini tarehe 17 na kurejea tarehe 21 Desemba
atatumia ziara hiyo kukutana na viongozi mbalimbali wa Serikali na wa makampuni
makubwa ili kujadili kwa pamoja namna pande mbili zitakavyoweza kushirikiana
katika miradi ya kipaumbele ambayo itarahisisha kwa haraka Serikali ya Awamu ya
Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kutimiza agenda ya uchumi
wa viwanda ifikapo mwaka 2020.
Waziri Mahiga na ujumbe wake utakaojumuisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na
Mipango wa Serikali ya Zanzibar, Bw. Khamisi Omari, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara
ya Kilimo, Dkt. Thomas Kashililah na Naibu Katibu Mkuu wa Biashara na Uwekezaji
kutoka Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Joseph Buchweishaija
wataiomba Serikali ya China kushirikiana na Tanzania kuendeleza miradi ya
kipaumbele katika sekta ya miuondombinu ya reli, viwanja vya ndege, bandari, nishati
ya umeme, maji na uwekezaji wa viwanda
Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa reli ya kati ambapo Serikali ya China imeonesha
dhamira ya kusaidia awamu zilizosalia. Aidha, licha ya Serikali ya awamu ya tano
kudhamiria kujenga kituo cha kuzalisha umeme wa Mega-Watts 2100 katika Mto Rufiji
(2100 MW Stigler’s Gorge Hydoropower project) kwa kutumia fedha za ndani lakini
Ujumbe huo utaiomba China isaidie mradi huo ili Serikali iweze kuokoa fedha na
kujikita katika miradi mingine.
Miradi mingine itakayojadiliwa ni pamoja na ujenzi wa Bwawa la Kidunda mkoani
Morogoro, Mradi wa ujenzi wa njia ya kusambaza umeme wa KV 400 kutoka Chalinze
hadi Dodoma, ukarabati wa Reli ya TAZARA na ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo
ambao upo katika hatua za mwisho za maandalizi ili uweze kuanza mapema mwakani.
Balozi Mahiga na ujumbe wake umepangiwa miadi ya kuonana na Waziri wa Mambo
ya Nje wa China, Mhe. Wang Yi, Naibu Waziri wa Biashara, Mhe. Qian Keming na
mmoja wa viongozi wa juu wa Chama Tawala cha China, State Councillor Yang Jiechi.
Waziri Mahiga pia atatembelea na kufanya mazungumzo na watendaji wakuu wa
makampuni makubwa ya China yakiwemo Sinolight ambayo pamoja na mambo
mengine inajihusisha na ununuzi wa mihogo mikavu, Kampuni ya Foton Motors
group inayotengeneza magari ya bei nafuu na kampuni ya China Merchant ambayo
inawekeza katika mradi wa Bandari ya Bagamoyo.
Kampuni zote hizo zimeonesha dhamira ya kufanya uwekezaji mkubwa hapa nchini
ambapo utakapokamilika utatoa ajira nyingi kwa Watanzania na kuongeza mapato ya
Serikali.
Ikumbukwe Waziri wa Mambo ya Nje wa China alifanya ziara ya kikazi hapa nchini
mwezi January 2017 ambapo alifanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa Serikali
akiwemo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim
Majaliwa. Mhe. Waziri Mkuu pamoja na mambo mengine aliishukuru China kwa
kuichagua Tanzania kuwa moja ya nchi 4 za Afrika zitakazonufaika na mpango wa
China wa kuhamishia baadhi ya viwanda vyake kwenye nchi hizo.
No comments:
Post a Comment