Mkuu wa wilaya ya Gairo, Siriel
Shaidi Mchembe amewataka wahitimu wa mafunzo ya mgambo kukiishi kiapo
cha utii kwa matendo na si maneno.
Hayo ameyazungumza leo Disemba
16, 2017 wakati wa hafla ya kuhitimisha mafunzo ya mgambo ambayo
yalifanyika katika Kata ya Rubeho halmashauri ya wilaya ya Gairo ambapo
mgeni rasmi aliwaasa wahitimu kutii yale yote waliyofundishwa ili
kujenga uchumi wa Taifa.
Katika hotuba yake Mhe. Mchembe
aliongeza kuwa mgambo wanapaswa kutumia elimu waliyoipata ili kuinua
uchumi wao na jamii inayowazunguka bila kuwaonea au kuwatesa wananchi.
“Nawaombeni sana ndugu zangu
mafunzo mliyoyapata ni muhimu sana katika taifa letu ni vyema sasa na
nyie mkayaishi yale yote mliyofundishwa kwa kipindi cha miezi mitatu
mliyoshiriki,” alisema Mhe. Mchembe.
Aliongeza kuwa ni vyema mgambo
wakawa mabalozi wema wa amani na si wao wawe mstari wa mbele katika
vitendo vya rushwa, unyanyasaji wa wananchi na kuepuka kujihusisha
kwenye uharifu kwa kukodisha magwanda yao.
Mhe. Mchembe aliwataka viongozi
wa wilaya kufanya usaili tena kwa wale mgambo wote ambao wameshapitisha
miaka 10 ili waweze kurudi kupata mafunzo zaidi.
“Kazi hii ya mgambo inahitaji
kuendelea kujifunza mara kwa mara hivyo nawaomba viongozi wote fanyeni
upya usaili wale wote ambao muda wa miaka 10 umepita warudie katika
mafunzo waweze kuongeza ujuzi zaidi,” alisema Mhe. Mchembe.
Alimalizia kwa kuwataka viongozi
wa wilaya kuwahamasisha akinamama kujitokeza zaidi katika mafunzo ya
mgambo maana idadi yao imeonekana kuwa ni ndogo sana ukilinganisha na
wanaume ambao wao wamekuwa mstari wa mbele katika kujitokeza.
Mafunzo hayo ya miezi mitatu
yalihitimishwa Disemba 13, 2017 yalisimamiwa na Mshauri Jeshi la Akiba
Gairo, Major Balitoga kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama
Wilaya ambapo jumla ya wahitimu 101 ambapo asilimia 11 tu walikuwa ni
wanawake.
Wahudhuriaji hafla hiyo walikuwa
ni Diwani wa Kata ya Rubeho Mhe. Digwagwala, Mtendaji wa Kata, Wenyeviti
wa vijiji, viongozi wa dini, wazee maarufu na wananchi zaidi ya 200
walishiriki maadhimisho hayo.
No comments:
Post a Comment