Msanii wa nyimbo za Injili aliyetamba
kwa vibao vyake murua na vyenye kuburudisha Rose Muhando, ametangaza
kujiunga rasmi na Chama cha Mapinduzi.
Msanii huyo ambaye aliomba kujiunga na
chama hicho amekabidhiwa kadi ya Chama cha Mapinduzi jana yeye pamoja na
kikundi chake, katika Mkutano Mkuu Maalum wa Tisa wa CCM Taifa,
unaofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete, mjini Dodoma.
Rose Muhando kabla ya kukabidhiwa kadi
ya chama cha CCM alitumbuiza kwa kibao maalumu alichokiandaa kwa ajili
ya Rais John Pombe Magufuli ambacho amekipa jina la “Magufuli Tubebe”.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM,
Humphrey polepole alitangaza kuwa Rose Muhando pamoja na Kundi lake
wameomba kupewa nafasi ya kutumbuiza kwa wimbo huo maalumu pamoja na
kukabidhiwa kadi za CCM.
“Kundi la Ndugu Rose Muhando na yeye
mwenyewe niwakaribishe Jukwani kwa wimbo ambao wameutunga maalumu kwa
Ndugu Magufuli. Kundi hili walipokuwa wanakuja walikuwa na maombi
mawili, ombi la kwanza ni kupewa nafasi ya kuimba wimbo huu maalumu na
pili kujiunga rasmi na CCM,” amesema katibu wa Itikadi na Uenezi,
Humphrey Polepole.
No comments:
Post a Comment