Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mh.
Luhaga Mpina amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Yohana Budeba
kumsimamisha kazi mara moja Afisa wa Kitengo cha Doria na Udhibiti wa
Uvuvi wa mpakani katika Mkoa wa Kagera bwana Ayoub Ngoma kwa tuhuma za
kushiriki katika utoroshaji wa samaki wenye kilo 2530 kwenda nchini
Burundi zenye thamani ya shilingi 20,850,000/= hapo jana.
Akizungumza katika ofisi ya
Kitengo hicho iliyopo mjini Kagera, Mpina alisema mnamo tarehe
03/12/2017 majira ya Saa 03:00 asubuhi, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya
Wilaya ya Ngara ilikamata gari lenye namba za uasajili T 614 CLQ aina ya
Mitsubishi Canter likiwa limepakia samaki zenye uzito wa kilo 2,000
aina ya Sangara na kilo 530 wa aina ya Sato kwenye mpaka wa Murusagamba
wilayani Ngara.
“Katika kipindi cha uongozi
wangu, tayari nimesha waagiza Makatibu Wakuu waliopo katika Wizara yangu
kutembea na barua zilizozosainiwa za kusimamisha kazi watumishi wote
wanaohujumu jitihada za Serikali ibaki kujaza jina tu. Kwa sasa hatuna
hata nusu dakika ya uvumilivu kwa watu kama hawa, tutawaondoa mara
moja.” Alisisitiza Mpina
Aidha, Waziri alisema Afisa huyo
na Dereva wa gari hilo bwana Ayuob Sanga wanashikiliwa na polisi kwa
hatua za kisheria kwa kuhusika na tukio hilo, na kuongeza kwamba samaki
hawa walikuwa wakitoroshwa kwenda nje ya nchi bila ya kufuata Sheria ya
Uvuvi Na 22 ya 2003 na taratibu mbalimbali za usafirishaji wa samaki na
mazao yake nje ya nchi.
Afisa Mfawidhi wa Kanda wa
Kitengo cha Doria na Udhibiti wa Uvuvi wa mpakani katika Mkoa wa Kagera
bwana Gabrieli Mageni alimweleza Waziri Mpina baadhi ya taratibu
zilizokiukwa kuwa ni pamoja na samaki hao kutopaswa kuvuliwa kwa kuwa
walikuwa wakubwa zaidi ya sentimeta 85 na wadogo chini ya sentimeta 50,
msafirishaji kutokuwa na kibali cha kusafirisha mazao ya uvuvi,
kutolipia ushuru na mrabaha wa Serikali, kutokuwa na cheti cha afya
pamoja na leseni ya kuuza mazao ya uvuvi nje ya nchi.
Waziri Mpina alisema samaki hao
walitaifishwa na kugawanywa kwa wananchi wa Murusagamba, Kiteule cha
Jeshi la Wananchi la Tanzania Murusagamba, Kituo cha Polisi Murusagamba
pamoja na Shule ya Sekondari Murusagamba baada ya kupata kibali cha
Mahakama.
Alisema kazi hiyo ilifanyika
chini ya usimamizi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya
ya Ngara. Luteni kanali,Michael Mtenjele. Aliongeza kuwa, uchunguzi wa
awali ilibaini kuwa samaki hao walitokea kwenye kijiji cha Izigo
wilayani Muleba.
Ametaja baadhi ya matukio
yaliyotokea hivi karibuni kuwa ni pamoja na kukamatwa kwa furu kilo
9100 zilizokuwa zinatoroshwa kwenda nchini Uganda ambapo zilitaifishwa
na kuuzwa kwa amri ya mahakama na watuhumiwa wawili kufikishwa
mahakamani kwa kosa hilo.
Kukamatwa kwa uduvi kilo 5000
ambazo zililipiwa mrabaha na mtuhumiwa kulipa faini ya shilingi
100,000/=,kukamatwa kwa mafurushi 6 ya Samaki aina ya Migebuka yenye
kilo 240 katika kituo cha Basi cha Bukoba zilizokuwa zikitoka mkoani
Kigoma kwenda Uganda ambapo mtuhumiwa alikimbia na samaki hao
kutaifishwa.
Katika tukio jingine jumla ya
kilo 100 za mabondo mabichi ya samaki yamekamatwa kwenye doria mpakani
Mtukula na mtuhumiwa amefikishwa polisi kwa hatua za kisheria.
Waziri Mpina amewaomba wavuvi
kuzingatia Sheria na taratibu mbalimbali za uvuvi nchini ili sekta hiyo
iwe na tija na kuchangia katika uchumi wa kati wa viwanda ifikapo
2025.
Wakichangia kwa nyakati tofauti
watumishi wa kituo hicho waliiomba Serikali kupitia kwa Waziri Mpina
kuangalia namna ya kuongeza nguvu kazi na vitendea kazi mbalimbali
vitakavyosaidia kudhibiti uvuvi haramu.
Nahodha Mkuu wa kituo hicho,
bwana Ernest Maguzu alisema kazi ya doria katika ziwa Viktoria imekuwa
ngumu kutokana na maendeleo makubwa ya teknolojia ya mawasiliano kwa
kuwa wavuvi wamekuwa wakiwasiliana mara moja kutumia simu za mikononi
pindi wanapoziona boti za doria zinaingia ziwani na kufanikiwa kukimbia.
Naye Kaimu Afisa Mfawidhi wa
Kitengo cha Udhibiti wa Ubora na Masoko bi, Theresia Temu aliiomba
kuongeza udhibiti wa usafirishaji wa bidaa zitokanazo na mazao ya uvuvi
nje ya nchi kwa kuwa hivi sasa Serikali imekuwa ikipoteza fedha nyingi
kutokana na wafanyabiashara kutorosha mazao hayo mipakani bila kulipa
ushuru.
Bi Temu alisema kuwa inakadiriwa
kuwa zaidi ya tani mia moja ya mazao ya uvuvi yanatoroshwa kila mwezi
katika mipaka ya nchi jirani hivyo jitihada za pamoja baina ya wadau
mbalimbali zinahitajika ili kupambana na tatizo hili
“Mheshimiwa Waziri hili ni tatizo
kubwa tunaomba Serikali kuliangalia kwa jicho la tatu namna nyingine
tutaendelea kuibiwa” alisisitiza bi Temu
Waziri Mpina alisema
Halimashauri zote nchini zinatakiwa kushiriki kikamilifu katika kulinza
raslimali za majini na baharini kwa kuwa licha ya raslimali hizo
kutoa mchango mkubwa wa uchumi kwa taifa pia manufaa yake ni kwa faida
ya vizazi vya sasa na baadaye.
“Nataka suala la uvuvi wa mabomu
na nyavu za kukokota liwe historia katika nchi yetu. Tutaendelea
kuchukua hatua kali kwa yeyote atakaje tuhujumu” alisisitiza Mpina
No comments:
Post a Comment