Jeshi la polisi mkoani Mwanza linamshikilia mtu mmoja kwa kosa la kujifanya daktari, katika hospitali ya mkoa Sekou Toure.
Joseph Mbagata (25),mkazi wa mtaa wa Mabatini jijini humo amekamatwa
jana Desemba 18 na jeshi hilo baada ya kubainika kwamba sio
mwanataaluma na alikuwa akiwatapeli wagonjwa kwa kuwaomba hongo, kitendo
ambacho ni kosa kisheria.
Taarifa kutoka kwa jeshi hilo zimesema kwamba mtuhumiwa alikuwa
akiwaomba hongo, huku akiahidi kuleta dawa muhimu na pia kufanya mipango
ili mgonjwa apate huduma kwa haraka.
Awali zilipatikana taarifa kuwa siku chache zilizopita alionekana mtu
aliyevalia mavazi ya udaktari na kujifanya daktari, kisha anapita wodini
kuwaona wagonjwa. Pia ilisemekana kuwa mtu huyo tayari amechukua
Sh30,000 kwa mgonjwa ili aweze kumpatia matibabu.
Aidha baada ya tuhuma hizo kufika katika uongozi wa hospitali waliweka
mtego na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa, akiwa amevalia mavazi ya
udaktari huku akiwa amesimama nje ya wodi ya upasuaji.
“Tumekuwa tukilalamikiwa kwamba kuna baadhi ya madaktari hapa hawana
ujuzi wala hawajitambui, kumbe ni dhahiri kwamba hao watu wapo na
kuanzia sasa lazima tufanye ukaguzi wa hali ya juu ili hali hiyo isije
ikajitokeza tena maana ni sehemu ya kuhatarisha maisha,” amesema mmoja
wa madakatri katika hospitali hiyo ambaye hakutaka kutajwa majina.
Baada ya daktari huyo feki kukamatwa, uongozi wa hospitali ulitoa
taarifa polisi, ambapo askari walifika eneo la tukio na kumuweka
mtuhumiwa chini ya ulinzi kisha kumfanyia upekuzi kwenye begi alilobeba
na kukuta mavazi yanayotumiwa na madaktari katika vyumba vya upasuaji.
Polisi wapo katika upelelezi na mahojiano na mtuhumiwa pindi uchunguzi
ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani ili hatua stahiki za
kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yake.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza naibu kamishina wa polisi Ahmed Msangi
ametoa wito kwa wananchi hususani wagonjwa waliopo hospitalini akiwaomba
kuwa makini na watu ambao ni matapeli wa aina kama hiyo wenye nia ovu
dhidi yao.
Aidha pia aliwaomba viongozi wa hospitali zote kuendelea kutoa taarifa
kwa polisi kuhusiana na watu wanao watilia shaka hospitalini, ili waweze
kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
No comments:
Post a Comment