Bunge la Afrika Mashariki (Eala) limemchagua Spika kutoka Rwanda, Dk
Martin Ngoga katika uchaguzi ulioibua mabishano ya kisheria juu ya
uhalali wa kufanyika kwake.
Baada ya dua ya kuliombea Bunge, mbunge Dk Ngwaru Maghembe kutoka
Tanzania aliomba mwongozo wa kuliahirisha kutokana na akidi kutotimia
kutokana na wabunge tisa wa Burundi na saba wa Tanzania kutokuwepo kwa
sababu ambazo hazikujulikana.
Mbunge kutoka Uganda, Freddy Mbidde alipinga hoja hiyo akisema kanuni ya
53(1) inayozungumzia akidi inahusu Bunge rasmi ambalo tayari lina Spika
lakini kwa kuwa hawakuwa na Spika kanuni hiyo haina nguvu kisheria.
Mbunge mwingine wa Tanzania, Dk Abdullah Makame alisema kutokana na
Bunge kuchelewa kuanza kazi kwa kipindi cha miezi sita kutokana na
mwanachama wa EAC nchi ya Kenya kuchelewa kuchagua wabunge ni busara
uchaguzi usifanyike hadi wabunge wote wawepo.
Hoja hiyo ilipingwa na mbunge kutoka Uganda, Suzane Nakauki aliyedai
hoja ya kutokufanya uchaguzi kwa sababu ya wabunge kutokuwepo haina
mashiko kisheria na kikanuni kwa sababu wameorodhesha majina yao kwenye
kitabu cha mahudhurio na wamepewa posho na wameamua kwa sababu
zisizojulikana kugomea uchaguzi.
Alisema haiwezekani wabunge wa Tanzania ambao wapo nchi mwao washindwe
kuhudhuria kikao cha Bunge wakati wapo jijini Arusha, huku waliotoka
mbali wakiwepo.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Balozi Liberat
Mfumukeko alisema kila jambo lenye mgogoro kwenye mihimili ya EAC lina
utaratibu wa kulimaliza kwa njia ya kuomba ushauri kwa sekretariati,
Mahakama, baraza la mawaziri na kikao cha marais.
Hatua hiyo ilimwinua Waziri wa Afrika Mashariki wa Burundi, Isabella
Ndahayo aliyesema wabunge wa Burundi hawakuridhishwa na utaratibu wa
uchaguzi licha ya kanuni kutamka wazi nafasi ya Spika ni ya mzunguko kwa
nchi wanachama.
"Wabunge wa Burundi hawapo kwa sababu hawaridhiki na kinachoendelea,
naomba tupewe tafsiri ya nafasi ya Spika kuwa ni mzunguko kwa nchi
wanachama, si kwamba tunapinga juhudi za mshikamano wa jumuiya bali
tafsiri halisi," alisema Isabella.
Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Uganda ambayo ni
Mwenyekiti wa EAC, Julius Wandera alisema kumekuwa na mashauriano kati
ya baraza la mawaziri wa jumuiya hiyo ili kuhakikisha suala hilo
linakamilika.
Baada ya mabishano ya kisheria na kanuni, katibu wa bunge aliamua
uchaguzi kufanyika na awamu ya kwanza, mgombea kutoka Rwanda, Dk Martin
Ngoga alipata kura 35, Leontine Nzeyimana wa Burundi kura moja na Adam
Kimbisa wa Tanzania hakupata kura.
Kutokana na kanuni kuhitaji mshindi kupata theluthi mbili ya kura zote
52, uchaguzi ulirudiwa kwa kanuni ya mshindi kupatikana kwa wingi wa
kura na Dk Ngoga aliibuka mshindi kwa kupata kura 33 dhidi kura tatu za
Nzeyimana ambaye hakuwepo bungeni.
Baada ya kula kiapo Dk Ngoga ambaye alikuwa mwendesha mashtaka mkuu wa
Rwanda alisema anafahamu uchaguzi wowote lazima uache majeraha lakini
yupo tayari kushirikiana na kila mbunge kujenga jumuiya hiyo.
No comments:
Post a Comment