KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka
ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela amewataka
madereva wanaoendesha magari ya zimamoto na uokoaji kwenye viwanja vyote
vya ndege Tanzania kuyathamini na kuyatunza magari hayo kwa kuwa
wameaminiwa kufanya kazi hiyo.
Bw. Mayongela alitoa kauli hiyo
kwenye Kituo cha Zimamoto na Uokoaji cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa
cha Julius Nyerere (JNIA), alipokwenda kujitambulisha na kujadili
changamoto mbalimbali zinazowakabili, ambapo alisema magari hayo
yamenunuliwa kwa gharama kubwa, hivyo yanapaswa kutunzwa.
Alisema uthamini wao kwa magari
hayo kutayafanya kudumu na kuyafanya kazi kwa muda mrefu bila
kuharibika, jambo ambalo litachangia ufanisi wa kazi, ya uokoaji na
usalama kwenye viwanja vya ndege, ambapo mbali na miundombinu pia lazima
miundombinu ipewe kipaumbele.
“Najua wapo wenzenu wachache sio
waaminifu wamekuwa wakitengeneza manunuzi hewa ya vifaa na hata mafuta
kwa manufaa yao binafsi, lakini ninawaomba mujione nyie ndio wenye
thamani kwa kuaminiwa kuendesha magari haya ya mamilioni ya fedha, kwani
ni nyie tu mnayoweza kuyaendesha kutokana na kuwa na mitambo ya kisasa
tofauti kidogo na mengine, hivyo basi tuyatunze ili tuisaidie serikali
yetu isiingie gharama za mara kwa mara za kununua vifaa au magari
mengine mapya,” alisisitiza Bw. Mayongela.
Hatahivyo, alisema zimamoto ni
moja ya mambo ya msingi hivyo amewahakikishia kuwapeleka kozi za mara
kwa mara za ndani na nje ya nchi, kutokana na mambo mbalimbali
yanayobadilika duniani, na kwa kuanzia ataanza na askari wawili hadi
wanne, kulingana na mafunzo wanayostahili kushiriki, na atahakikisha
washiriki ndio wanaokwenda kufanyia kazi kwa vitendo katika utendaji wao
na sio kupeleka mabosi ambao hawahusiki.
“Nia yangu ni nyie kufanya kazi
kwa weledi na kufanyakazi kwa bidii, nisije kusikia hakuna fedha, lakini
wakati huo huo mnamuona Mkurugenzi mkuu anapanda ndege kwenda Ulaya na
kurudi hizo fedha zinatoka wapi, nasema kama kweli kuna mambo ya msingi
basi zimamoto ni jambo la msingi, hivyo basi sisi wafanya maamuzi
tunatakiwa kuangalia wanaostahili kupata mafunzo na waende, hivyo
nitahakikikisha kwa kadri ya bajeti nitatenga mafungu ya kupeleka watu
wangu hawa kwenye mafunzo, ili nao waende na wakati katika endeshaji
kulingana na mabadiliko ya teknolojia na mashirika ya usafiri wa anga
duniani yanavyoagiza,” alisema Bw. Mayongela.
No comments:
Post a Comment