WAZIRI
wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo
na Balozi wa Norway hapa nchini Bi. Hanne-Marie Kaarstad na kutoa wito
kwa wawekezaji kutoka Norway kuja kuwekeza Tanzania katika sekta
mbalimbali zikiwemo Nishati, misitu, kilimo, gesi na mafuta.
Dkt.
Mpango amemweleza Balozi huyo kwamba Tanzania iko katika hatua
mbalimbali za kukuza uchumi wake kupitia sekta ya viwanda na kwamba
wawekezaji kutoka Norway watakuwa na mchango mkubwa wa kuiwezesha
Tanzania kufikia lengo hilo.
Aliyataja
maeneo ya kuongeza thamani ya mazao ya misitu, mifugo, uvuvi, nishati,
kilimo na mengine mengi kwamba yataongeza tija katika sekta hiyo na
kwamba malighafi za kilimo zitatochea uzalishaji katika viwanda na
kuinua kipato cha wananchi.
“Tumeamua
kujenga Reli ya Kati kwa viwango vya kimataifa-SGR ambayo inahitaji
umeme wa kutosha kwa hiyo bado tunahitaji mchango wa wadau mbalimbali
ikiwemo Norway ili kuhakikisha kuwa tunakuwa na nishati ya umeme ya
kutosha na ya uhakika ili kufanikisha mradi huo mkubwa” aliongeza Dkt.
Mpango
Kuhusu
Sekta Binafsi, Dkt. Mpango amesema kuwa Serikali imeendelea na
majadiliano na Sekta hiyo ili kutatua changamoto mbalimbali
zinazoikabili ikiwemo masuala ya kodi pamoja na kujenga kuaminiana kati
ya pande hizo mbili.
Amefafanua
kuwa Sekta Binafsi ni muhimu katika ukuaji wa uchumi wa Taifa na kwamba
vikao hivyo vya mara kwa mara vimeanza kuzaa matunda.
Ameishukuru
nchi ya Norway kwa mchango mkubwa wa maendeleo kwa kusaidia kuboresha
masuala ya nishati, kilimo, uboreshaji wa mifumo ya kodi kupitia Mamlaka
ya Mapato Tanzania TRA, kuchangia fedha katika program ya Maboresho ya
Usimamizi wa Fedha za Umma na kuchangia Bajeti Kuu ya Serikali kila
mwaka.
Kwa
upande wake Balozi wa Norway hapa nchini Bi. Hanne-Marie Kaarstad
alisema nchi yake imeridhika na namna Serikali ya Awamu ya Tano
inavyopiga hatua kubwa katika maendeleo ya watu wake kupitia kuhamasisha
uchumi wa viwanda.
Amesema
kuwa nchi yake imesaini mikataba mikubwa miwili hivi karibuni ukiwemo
mkataba wa msaada wa krona milioni 600 (fedha za Norway) kwa ajili ya
mradi wa kusambaza umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati
Vijijini-REA, hatua anayoamini kuwa itaharakisha maendeleo na uchumi wa
kati wa wa nchi ifikapo mwaka 2025 na kuongeza kuwa nchi yake
itaendeleza uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi hizo mbili.
Amesisitiza
umuhimu wa Serikali kuishirikisha kikamilifu Sekta Binafsi katika hatua
yoyote inayopiga kuelekea maendeleo ya haraka kwa kuwa sekta hiyo ina
mchango mkubwa katika kufikia mafanikio tarajiwa.
Aliahidi
kuendelea kuhamasisha wawekezaji kutoka nchini mwake kuja kuwekeza
Tanzania na kushauri kuwa wakati mambo hayo yakiendelea, Tanzania
ihakikishe kuwa sera zake za uchumi zinakuwa imara na
hazibadilikibadiliki ili wawekezaji waweze kuamini wako salama.
Alishauri
kuwa kila aina ya mabadiliko katika sera za nchi yakiwemo masuala ya
kodi yanapaswa kuwa shirikishi ili sekta hiyo iweze kutoa mchango wake
kikamilifu baada ya kushirikishwa katika maamuzi mbalimbali na kupongeza
hatua ya Serikali ya kukutana na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi
kujadiliana kuhusu masuala mtambuka.
No comments:
Post a Comment