Shughuli ya kusukwa upya kwa safu ya
uongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania itahitimishwa wiki
hii katika mkutano mkuu unaofanyika mjini Dodoma, katikati mwa nchi
hiyo.
Huu ni uchaguzi wa kwanza tangu Rais John Magufuli aliporithi uenyekiti kutoka kwa mtangulizi wake, Jakaya Kikwete.
CCM inaendeleza mikakati ya kurejesha hadhi yake baada ya ushindi uchaguzi wa mwaka 2015.
Licha
ya kushinda urais kwa taabu, wapinzani chini ya mwamvuli wa UKAWA
walipata karibu theluthi moja ya viti vyote vya ubunge na kudhibiti
halmashauri katika miji muhimu ikiwemo Dar es Salaam, hii ikiwa ni
rekodi mpya.
Miaka miwili ndani ya utawala wa Rais Magufuli, upepo unaonekana kugeuka.
Upinzani unaelekea kudhoofika, wakati CCM ikiimarika na kung'ara miongoni vyama vya ukombozi vilivyoleta uhuru katika nchi zao.
Ingawa
haikuwepo wakati wa uhuru wa Tanganyika mwaka 1961 wala mapinduzi ya
Zanzibar 1964, CCM inahesabika kama chama cha ukombozi kwa sababu
kilizaliwa na vyama viwili vyenye sifa hiyo, TANU ya Tanganyika na ASP
ya Zanzibar chini ya waasisi Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Abeid
Amani Karume.
Wakati CCM ikizidi kuimarika, vyama vingi
vilivyoanzishwa katika miaka ya 1950 na 60 vilishatimuliwa madarakani,
vikiwemo United National Independence Party (UNIP), Malawi Congress
Party (MCP) na Kenya African National Union, (KANU).
UNIP ya
Kenneth Kaunda ilikuwa ya kwanza kuangushwa mwaka 1991 baada ya miaka 27
madarakani, ikafuatiwa na MCP ya Kamuzu Banda mwaka 1994 (miaka 29
madarakani) na kisha mwaka 2002 ikawa zamu ya KANU (miaka 39
madarakani).
Baadhi ya vyama vya ukombozi kama Parmehutu cha
Rwanda, Mouvement National Congolais (MNC) cha Kongo- Kinshasa
vilishafutwa miaka mingi.
Nini siri ya nguvu ya CCM?
Siri
ya kwanza ya nguvu ya CCM ni Nyerere, Rais wa kwanza ambaye Watanzania
wanamkumbuka kwa mapenzi makubwa wakimuita 'Mwalimu, au 'Baba wa
Taifa.' Anaweza kuwa hakufanikiwa sana katika nyanja ya uchumi, lakini
Nyerere alijenga taifa na kuwaunganisha Watanzania.
Pia, Nyerere
alijijengea heshima kwa kung'atuka mwenyewe madarakani akiwa bado ana
nguvu na kusimamia mchakato wa kumpata mrithi wake, kinyume na wengine
waliosubiri watolewe.
Nchi chache zina watu wa hadhi ya Nyerere na Nelson Mandela wa Afrika ya Kusini.
Hakuna kati ya Jomo Kenyatta wa Kenya, Dkt Hastings Kamuzu Banda wa
Malawi wala Kenneth Kaunda, aliyewahi hata kupokonywa uraia wa Zambia,
anayeheshimiwa katika nchi zao kama anavyoheshimiwa Nyerere.
Kutokana
na mapenzi ya Watanzania kwa Nyerere na CCM yake, haikushangaza kwamba,
mwaka 1991, matokeo ya Tume ya Rais iliyopewa jukumu la kukusanya maoni
ya Watanzania juu ya mfumo wa vyama yalionesha kuwa asilimia 80 ya
Watanzania walitaka chama kimoja kiendelee.
Bahati nzuri, mwenyewe aliunga mkono mfumo wa vyama vingi na sauti yake ikawa kura ya turufu.
Hata hivyo, wananchi wengi hadi sasa wanaiona CCM kama urithi wa Mwalimu hivyo kuasi chama hicho ni usaliti wa kumbukumbu yake.
Hii
inaonesha kuwa vyama vingi si mtindo wa maisha ya kisiasa uliochaguliwa
na Watanzania, bali ulianzishwa kwa sababu ilikuwa 'fasheni' ya wakati
ule katika siasa mpya za dunia baada ya kudondoka kambi ya Mashariki ya
Wajamaa.
Katika hali hii, uzoefu wa miaka 25 wa siasa za vyama
vingi unaonesha kuwa Watanzania wanavitumia vyama vya upinzani kama
mahali pa kuonesha hasira zao pale serikali ya CCM inaposhindwa kukidhi
matarajio yao katika kusimamia uchumi na kupambana na ufisadi.
Kwa lugha za mtaani, CCM ni mke, upinzani ni kimada.
Wimbi
la hivi karibuni la viongozi wa upinzani kuhamia au kurudi CCM na kudai
kuwa hakuna haja ya upinzani kwa sababu ya mafanikio ya Rais Magufuli
inathibitisha nadharia hii.
Demokrasia ndani ya chama
CCM
ukilinganisha na kizazi cha vyama vyenzake vya ukombozi vilivyotimuliwa
madarakani imekuwa ina demokrasia pana ya ndani ya chama na mifumo
madhubuti ya kutatua migogoro na hivyo kukiwezesha kuhimili misukosuko.
Baada ya Nyerere kung'atuka, kumekuwa na kupokezana madaraka kwa marais watano mpaka sasa.
Kadhalika
CCM imeweza kuvuka salama nyakati ngumu ikiwemo madai ya Serikali ya
Tanganyika yaliyoibuliwa na wabunge 55 mwaka 1993 na shinikizo la
wajumbe wa vikao vya halmashauri kuu na mkutano mkuu uchaguzi mkuu
uliopita (2015) waliotaka Edward Lowassa awe mgombea urais wa chama
hicho.
Ukiangalia vyama vya ukombozi katika nchi nyingine,
vingi viliponzwa na ukosefu wa demokrasia na uwezo mdogo wa
kushughulikia migogoro ya ndani.
KANU iliponzwa na Rais Daniel arap Moi aliyejaribu kuwachagulia Wakenya mrithi.
Naye, Dkt Banda wa Malawi alishajikabidhi uenyekiti wa chama na urais wa maisha wa nchi yake.
Wawili hawa walipalilia uasi ndani ya vyama vyao.
Huenda
kiongozi mpya wa ANC, atakayemrithi Jacob Zuma atahitaji somo kutoka
CCM kuepusha chama chake na zahma iliyovikumba vyama hivi.
ANC,
kama CCM inajivunia muasisi, Nelson Mandela na uimara wa kitaasisi,
lakini inahitaji Magufuli wake wa kufungua ukurasa mpya kwa ajili ya
Afrika ya Kusini.
Mustakabali wa CCM mpya
Baada
ya kupitia kipindi kigumu cha kushuka umaarufu wake hususan katika
awamu ya pili ya uongozi wa Rais Kikwete, CCM inaelekea kurejesha hadhi
yake, ikisaidiwa na faida ya mifumo imara wa uendeshaji wa chama,
demokrasia ya ndani na historia iliyotukuka inayofungamanishwa na
umaarufu wa muasisi wake.
Hata hivyo, kwa upande mwingine, hadhi ya CCM inarejea kwa gharama
kubwa kwa demokrasia changa ya Tanzania. Katika siku za hivi karibuni
madiwani na wabunge wa upinzani wamekuwa wakihama vyama vyao kwa madai
kuwa Rais Magufuli anafanya kazi nzuri.
Hata hivyo, wapinzani wanadai rushwa imekuwa ikitumika kuwashawishi wahamie CCM.
Kama hiyo haitoshi, Rais Magufuli amekuja na maagizo mapya juu ya namna ya kufanya siasa.
Hakutakuwa tena na mikutano ya siasa ya hadhara mpaka wakati wa uchaguzi isipokuwa kwa wabunge na madiwani katika maeneo yao.
Wakati huohuo, Rais Magufuli mwenyewe anafanya mikutano kama kawaida akichanganya shughuli za chama na serikali.
Kadhalika,
viongozi wa upinzani wamejikuta matatani wakikamatwa na kushtakiwa kwa
uchochezi pale wanapotoa matamshi mbalimbali, huku wengine wakihofia
usalama wao baada ya kupokea vitisho.
Kwa ujumla tutegemee CCM mpya ya Magufuli kuimarika zaidi, lakini pia tutegemee kudorora kwa upinzani.
Si
ajabu kwamba, baada ya miaka mitano ya Rais Magufuli, vyama vyaupinzani
vitarejea katika hali yao ya miaka ya 1990 wakati wakipigania haki za
msingi za kidemokrasia, badala ya kuzungumzia miradi ya maendeleo,
mbadala wa ile ya CCM.
No comments:
Post a Comment