Juhudi za kuwapata watu wanne wanaodaiwa kumbaka na kumjeruhi mama mmoja mkazi wa Manispaa ya Musoma zimegonga mwamba baada ya watu hao kukimbilia kwenye bwawa la Kitaji lililopo Musoma kwa lengo la kujificha.
Watu hao wanaodaiwa kukimbilia bwawani humo jana Juni 19, 2023 kwa lengo la kujificha walitafutwa siku nzima na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji bila mafanikio.
Akizungumzia tukio hilo leo Jumanne Juni 20, 2023, Kamanda wa jeshi hilo mkoani Mara, Agostino Magere amesema hadi wanaondoka katika eneo la tukio jana saa 1.40 usiku hakuna mtu yeyote aliyepatikana katika bwawa hilo.
“Jana changamoto kubwa ilikuwa ni mazingira ya bwawa kwa ujumla kuna matope, magugu na kina kirefu nyasi zimeota kiasi kwamba inakuwa ni vigumu kuingia mle ndani,”amesema
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Kelvin Onyango amesema vijana sita wanadaiwa kumbaka mwanamke mmoja asubuhi na kisha kukimbilia kwenye bwawa hilo baada ya kukimbizwa na wananchi.
“Walikuwa watu kama sita hivi wawili wakaelekea upande wa kule wanne baada ya kuona wamezingirwa wakaingia humu bwawani sasa tangu wameingia hawajatoka,”amesema.
Mwita Wambura amesema kuwa kazi ya kuwatoa watuhumiwa hao kwenye bwawa hilo ilikuwa ngumu kutokana na mazingira ya bwawa hilo ambalo limefunikwa na magugu.
“Hapa kuna magugu maji yamefunika bwawa zima lakini pia chini kuna tope sasa inakuwa ni vigumu kuingia majini,kwahiyo hawa wazamiaji wanashindwa,” amesema
Akisimulia tukio la ubakaji lilivyotokea, Majura Johnson amesema asubuhi akiwa anaelekea kazini alisikia sauti ya mama ikilia kuomba msaada kutokea kwenye jumba bovu liliopo pembezoni mwa barabara ya Serengeti Manispaa ya Musoma.
Amesema alipofika kwenye eneo hilo aliwakuta vijana sita mmoja akiwa uchi wa mnyama wakimbaka mama huyo na baada ya kumuona walikurupuka na kuanza kukimbia.
No comments:
Post a Comment