Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita imeelezwa kuwa mshtakiwa Elpidius Edward anayedaiwa kuvamia Kanisa Kuu la Kiaskofu jimbo Katoliki Geita na kufanya uharibifu uliosabisha hasara ya Sh48.2 milioni hana tatizo la afya ya akili.
Akitoa ushahidi mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Johari Kijuwile Shahidi wa upande wa mashtaka ambaye ni daktari kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita, Christopher Matola ameieleza Mahakama kuwa vipimo alivyomfanyia mshatakiwa vilionyesha ana akili timamu.
Shahidi huyo ameieleza Mahakama kuwa alimfanyia uchunguzi wa afya ya akili mshtakiwa kwa zaidi ya saa mbili kwa kumuuliza maswali ya mazingira, aina ya watu anaowaona pamoja na kumtaka ajitambulishe na kwamba maswali yote aliyajibu kwa ufasaha.
Kufuatia majibu aliyoyatoa mshtakiwa, yalimpa nafasi Dk Matola kujiridhisha kuwa hana tatizo la akili na kuwa alimweleza kabla ya kwenda kanisani alikuwa akinywa pombe na rafiki yake eneo la Pinpoint mjini Geita na kisha kwenda nyumbani kwa rafiki yake eneo la Kisesa.
Shahidi mwingine, Erick Herman ambaye ni msimamizi wa walinzi wanaolinda eneo la Kanisa kuu la kiaskofu jimbo Katoliki la Geita ameieleza Mahakama kuwa siku ya tukio akiwa eneo lake la kazi alimuona mshtakiwa akivunja vitu ndani ya Kanisa.
Mshatakiwa Elpidius, Mkazi wa Geita anashtakiwa kwa makosa mawili ikiwemo la kuingia katika jengo la Kanisa Katoliki Geita kinyume na kifungu cha 294 (1) na (2) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Katika shtaka la pili mshtakiwa huyo anadaiwa kuharibu mali zenye thamani ya Sh48.2 milioni kinyume na kifungu namba 226 (1) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Kesi hiyo namba 62/2023 imeahirishwa hadi Julai 3, 2023 itakapokuja kwa ajili ya upande wa mashtaka kuendelea kutoa ushahidi huku mshatakiwa akirejeshwa mahabusu kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana yaliyomtaka kuwa na wadhamini wawili watakaosaini hati ya fedha taslimu Sh24.1 milioni au mali isiyo hamishika yenye thamani hiyo.
No comments:
Post a Comment