Wakati mwili wa mwimbaji wa kwaya ya
Vijana ya Kanisa la AICT, Chang’ombe jijini Dar es Salaam, Mariam
Charles ukizikwa kwenye makaburi ya Maduka Mawili-Chang’ombe jana, mtu
anayedaiwa kumuua amekamatwa na polisi kwenye nyumba ya wageni iliyo
jirani na kanisa hilo maeneo ya Sokota.
Akielezea namna mtuhumiwa huyo
alivyokamatwa, meneja wa nyumba ya kulala wageni ya Kisuma iliyopo
maeneo ya Sokota-Chang’ombe, Damian Urio alisema mtuhumiwa ambaye
alijiandikisha kwa jina la Frank Magulu alifika katika nyumba hiyo ya
wageni ambayo inapakana na kanisa la AICT juzi jioni.
Urio alisema baada ya mteja huyo kufika katika ‘gesti’ hiyo, mhudumu alimpangisha chumba namba 230 alimolala hadi jana asubuhi.
“Alikuja jana (juzi) japo majira
sikumbuki vizuri, lakini alifika akapewa chumba. Aliingia na baadaye
akatoka kidogo, hakukaa sana akarudi kulala,” alisema Urio.
Alisema kwa kuwa hawakujua chochote walimhudumia kama wateja wengine.
“Leo hii (jana) saa tano mhudumu
alimgongea chumbani akamwambia atoke afanye usafi. Lakini mteja aliomba
maji ya kopo akaambiwa mbona bafuni yapo? akasema anataka hayo, basi
akapewa na kunawa.”
Alisema baada ya kunawa alitoka kwenda
kutafuta chai na aliporudi akaingia tena chumbani, lakini alionekana
kama amechanganyikiwa kwa kuwa alikuwa hatulii. “Basi alitoka chumbani
akaja mapokezi wakati anaongea ghafla tukashangaa polisi wameingia na
kumkamata,” alisema Urio.
“Kwenye kitabu jana aliandika jina lake kamili la Frank Magulu analotumia, lakini alikuwa kama hana raha.”
Wakati mtuhumiwa huyo akikamatwa na
polisi gesti, upande wa pili kama mwendo wa dakika moja lilipo kanisa la
AICT, ibada ya kumuaga Mariam ilikuwa ikiendelea.
Polisi waelezea
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke,
Emmanuel Lukula amesema jana walifanikiwa kumtia mtuhumiwa mbaroni
wakati akijiandaa kuingia nyumba ya kulala wageni ya Kisuma iliyoko
maeneo ya Sokota.
Alisema kuwa walimpeleka hospitali ya
Temeke baada ya kuwaambia kuwa amekunywa vidonge kumi vya valium na
konyagi ili afe kama Mariam.
“Mtuhumiwa anafahamika kwa majina ya Nandi Joseph Magulu au Frank Joseph Magulu, miaka 29,” alisema.
Kamanda Lukula alisema mtuhumiwa huyo ni mtaalamu wa maabara na ni mkazi wa Kilakala, Temeke.
“Mtuhumiwa amekutwa na daftari aliloandika kujutia kumuua marehemu kwa wivu wa mapenzi,” alisema kamanda.
Shuhuda azungumza
Mmoja wa watu walioshuhudia kukamatwa
kwa mtuhumiwa huyo alisema huenda baada ya msiba angesababisha tukio
jingine kama alivyokuwa anasambaza ujumbe.
Shuhuda huyo ambaye ni mmoja wa
wanakwaya hao wanaotamba na albamu ya Pazia la Hekalu, alisema mtuhumiwa
alijiunga nao mwaka mmoja uliopita.
Alisema wakati anajiunga na kwaya hiyo alikuwa akitokea mkoani Shinyanga.
“Alijiunga na kwaya na kwa sababu hapa
kwetu kuna utaratibu wa kuhakikisha walau kijana awe na kazi alisaidiwa
na kupata kazi ya maabara kwa sababu ni fani yake,” alisema mwanakwaya
huyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.
Alisema wakati akiendelea na kazi
alidaiwa kumuibiwa mwajiri wake na kuamua kukimbia. “Kwa hiyo aliporudi
ndiyo sasa tukio hili likatokea, alikuwa kwenye mahusiano halali ya
uchumba na ukimuona hakuwa anaonyesha kama anaweza kufanya unyama huo,”
alisema.
Mwili wa Mariam (26), ulikutwa kwenye
nyumba ya wageni ya East London iliyopo Buza anakodaiwa alikuwa na
mchumba wake usiku wa kuamkia Jumatano.
Viongozi wa kanisa
Akihubiri jana katika ibada kanisani
hapo wakati wa kumuaga Mariam, mchungaji kiongozi wa kanisa hilo, Elisha
Isebuka alisema ilikuwa vigumu kupokea msiba huo na kwamba hakuamini
alipoelezwa na wazazi wa marehemu.
“Tunatambua Mariam alikuwa sehemu yetu
na leo hayupo. Hata hivyo tunamshukuru Mungu hata katika hili najua
tunapitishwa kwenye wakati mgumu ambao tunaweza kulaumu, lakini katika
yote Mungu atabaki kuwa Mungu,” alisisitiza.
Katibu wa kwaya aliyokuwa akiimba
Mariam, Dickson Seni alisema wanapitia katika huzuni kubwa ya kuondokewa
na mwenzao lakini hawana budi kumshukuru Mungu kwa jaribu hilo.
“Tutaendelea kumuenzi mwenzetu tukiwa
pamoja na wazazi wake, tumehuzunika sana lakini tunaamini hata katika
hili bado Mungu hatatuacha,” alisema Seni.
Askofu wa Kanisa la AICT Dayosisi ya
Pwani, Charles Salala alisema nyakati yanapotokea matukio ya kutisha
kama hilo ni wakati wa kumtafakari Mungu.
“Hili tuliache mikononi mwa Mungu mwenyewe na niwape pole wazazi, ndugu, wanakwaya wenzake na waumini wote,” alisema.
Akizungumzia tukio hilo juzi, mama mzazi
wa Mariam, Esther Lutonja alisema binti yake alimuaga kwenda kuonana na
mchumba wake mchana wa Jumanne na hakurudi. Baadaye, Ester alisema
Jumatano alitumiwa ujumbe mfupi wa simu na mchumba wa mwanaye uliosema,
“tayari nimemuua mwanao”.
Hata baada ya mwili wa Mariam kupatikana, mtuhumiwa alidaiwa kuendelea kutuma ujumbe wa vitisho kwa ndugu wa marehemu.
Ndugu hao walisema kuna wakati mtuhumiwa alitumia simu yake na wakati mwingine simu ya Mariam.
Akizungumzia ujumbe huo, dada wa Mariam,
Lucy Enock alisema baadhi ya wanafamilia wametumiwa ujumbe wa vitisho
kwa simu aliyokuwa anatumia mdogo wake.
Alisema ametumiwa ujumbe kwa namba ya Mariam unaosema:
“Nimemuua Mariam kwa ajili ya uongo wake
kwangu na alinitengenezea njama kwa mama Kashimba ili nikamatwe,
nikamgundua baada ya mama huyo kumpigia akiwa anaoga...”
Ndugu mwingine wa marehemu, Paul Makelele alisema amepokea vitisho kutoka kwenye namba ya Mariam.
“Kuna meseji nimetumiwa, inasema:
“Mtindo wako wa kushindwa kutunza siri nina silaha au nikufuate? Ni
meseji nyingi napokea,” alisema.
Meseji nyingine aliyotumiwa ilisema:
“Jamani kama kukimbia ningeweza, maana
nilikuwa nimefika nje ya mji, saa hivi nimerudi naenda polisi mwenyewe,
hata kujiua nashindwa hata nikijaribu kwa sababu sijaua kwa kukusudia,”
Ujumbe huo mfupi uliendelea kusema: “Ni
bora kuuliwa kuliko mateso ya nafsi ya Mariam ninayoyapata. Mariam
ananitokea kila nikitaka kujiua...”
Mauaji ya wenza
Akizungumzia tukio la aina hiyo, daktari
wa magonjwa ya akili kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk
Omari Ubuguyu alisema kisaikolojia kuna mambo mengi yanayomfanya mtu
aue.
Alisema mbali ya mambo hayo, yapo
mengine makuu matatu ambayo ni magonjwa ya akili, tatizo la kisaikolojia
na ya kijamii ikiwamo yanayoaminiwa na watu.
Dk Ubuguyu alifafanua kuwa katika magonjwa ya akili mtu anaweza kuwadhuru watu baada ya kupata hisia za kiugonjwa.
Alisema mtuhusika anaweza kudhani kuwa watu ni wabaya na wanapanga au wanaweza kumdhuru yeye, watu wa karibu au watu wengine.
“Kitaalamu hali hii huwa tunasema
wanarespond to psychotic experiences,” alisema. “Watu wenye ugonjwa
unaoitwa schizophrenia, delusional disorder (paranoid type) na baadhi ya
wagonjwa wa kifafa ni miongoni mwa watu wanaoonyesha kupatwa na shida
hii,” alisema Dk Ubuguyu. Mtaalamu wa saikolojia kutoka Muhimbili, Dk
Isack Lema alisema licha ya kuwapo kwa mambo mbalimbali yanayosababisha
hakuna la moja kwa moja linalohusishwa.
Alisema mtu hufanya hivyo kulingana na kinachomsukuma kwa wakati huo.
“Kwa kawaida anayefanya mauaji kwa hisia huwa ana tatizo la kiafya,” alisema Dk Lema.
“Sasa inaweza kuwa ya mwili,
kisaikolojia kutokana na mazingira aliyokulia kwa sababu hakuna binadamu
anazaliwa na dhamira ya kuua labda kama ameishi katika mazingira
hatarishi kama ya vita, hivyo amekata tamaa.”
No comments:
Post a Comment