Na Rhoda Ezekiel
Makamau wa Rais Samia Hassan amewataka
viongozi wa dini kuepuka kuchanganya dini na siasa na kujiepusha na
migogoro ya kiutawala ndani ya kanisa kwa kuwa kazi ya kanisa ni
kuhubiri amani kwa waumini.
Wito huo aliutoa leo katika ibada ya
uwekwaji wakfu maaskofu watano wa majimbo matano, katika kanisa la
Pentekoste Motomoto mjini Kigoma.
Aidha aliwataka maaskofu hao kufanya
kazi kwa kushirikiana na serikali kwa kuwa serikali itaendelea
kushirikiana nao katika kazi njema na kwamba ili kufikia maendeleo ni lazima kuhakikisha kuwa nchi yetu inaendelea kuwa na amani na utulivu.
"Kigoma ni mashuhuda wa athari za
ukosefu wa amani kwa kuwa mmepokea wakimbizi kutoka nchi jirani, ni
vyema kanisa likalinda amani ya nchi yetu, lazima kanisa lijiepushe na
migogoro ya kiutawala ndani ya kanisa",aliongeza Samia.
"Kazi kubwa ya kanisa ni kuhubiri amani
kwa waumini wake na wananchi kwa ujumla, neno la Mungu katika kitabu
cha Waebrania 12:14 linasema,tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu
wote , naomba muendelee kuhubiri amani kwa kuwa serikali haipendi kuona
mogogoro ya kidini ndani ya mashehebu, baina ya dhehebu na dini
nyingine", alisema Makamu wa Rais.
Hata hivyo alisema serikali inalitegemea
kanisa kujenga maadili ya jamii kwani vijana wengi wameiga tamaduni za
kigeni na kanisa liendelee kupiga vita tamaduni mbaya za nje ili kuwa
na kizazi chenye maadili mema.
Katika hatua nyingine aliwapongeza
viongozi wa Kanisa hilo kwa kulinda misitu na kuwaomba viongozi wengine
kuendelea kutunza mazingira kwa kuwa maeneo mengi yameharibiwa kutokana
na watu kukata miti na wote watakaofanya hivyo watasaidia mazingira
kuhifadhiwa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa kigoma Brigedia
Jenerali Emmanuel Maganga alitumia mkutano huo kutoa wito kwa wanaume
kutumia fursa ya kwenda kupima afya na kujua afya kwa ajili ya kujua
afya na kuanza kula chakula chenye lishe ili kuweza kuwa na nguvu na
kuweza kufanya kazi.
Alisema mkoa wa Kigoma una chakula cha
kutosha lakini ni moja kati ya mikoa yenye watu wenye utapiamlo pamoja
na chakula kilichopo na kuwaomba wananchi kufuata maelekezo ya wataalamu
wa afya kuhusiana na mlo unaojenga afya.
Kwa upande wake, Askofu mkuu wa Kanisa
la Pentekoste Motomoto Ezra Mtanya aliipongeza serikali kwa kazi nzuri
ya kuwaletea maendeleo wananchi pamoja na kuzuia wizi wa maliasili,
madini na kuwaibia wananchi uchumi wao, ambapo mambo hayo
yasingesimamiwa kwa umakini wananchi wangeweza kuhujumiwa na kukosa haki
yao.
Pia aliahidi kuwahimiza ananchi na
waumini kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia sera zilizopo, kwa kufanya
kazi pamoja na kuanzisha viwanda kwa mustakabali wa kuinua uchumi na
Maendeleo kwa wananchi.
Alisema kwa upande wa kanisa
linatekeleza sera ya uanzishwaji wa viwanda kwa kuweka mpango wa kufuga
nyuki, kwa kuwa mpaka sasa wanamiliki misitu katika wilaya ya Nzega na
Uvinza ili kuanza uzalishaji na wameiomba serikali kuwasaidia
kuwawezesha kiuchumi waweze kukamilisha mipango yao.
Aliwataka Maaskofu waliowekwa wakfu leo
kuongozwa na roho wa Mungu,na kuyatenda yale yote ambayo hayajafanyika
ili kuhakikisha kanisa linakuwa jema kwani wamekabidhiwa nafasi ya
ukuhani wa Mungu na wanatakiwa kusimamia haki na kuwafundisha waumini
neno la Mungu lililo la kweli na kuwa na umoja na ushirikiano.
Kwa niaba ya serikali Makamu wa Rais
amewapongeza maaskofu waliowekwa wakfu na kuwa maaskofu ambao Askofu
Bwami Mathias askofu mkuu msaidizi, Askafu Eliasaph Mathayo Eliasaph
Mathayo askofu jimbo la Mashariki, Askofu Simon Bikatagu jimbo la
Magharibi , Askofu Jackson Maneno Jimbo la Kusini, Askofu Shemu Mwenda
jimbo la Kati kwa kuchaguliwa kuongoza majimbo na kuitikia wito.
Makamu wa Rais Mama Samia Hassani
ameanza ziara yake mkoani Kigoma jana tarehe 08 Septemba na anatarajiwa
kufanya ziara ya siku nne ambapo anatarajia kumaliza ziara yake tarehe
11 Septemba 2018 kwa kuzungumza na Wananchi wa Buhigwe.
No comments:
Post a Comment