Watu huwa na imani tofauti na huabudu vitu vingi duniani.
Nchini Nigeria, kuna kabila moja ambalo humuabudu mamba kama miungu.
Mamba huyo wanayemuabudu kwa sasa ana umri wa miaka 78.
Wakazi wa eneo hilo la Oje viungani mwa mji wa Ibadan kusini
magharibi mwa Nigeria humuenzi mamba huyo sana na wanaamini kwamba mamba huyo
anaweza kujibu maombi yao.
Huwa wanamrushia kuku kama zawadi kumshawishi kutimiza
maombi yao, wengine humpa mbuzi.
Mamba huyo humilikiwa na familia ya Delesolu ambao wamekuwa
wakimfuga kama mnyama kipenzi.
Anadaiwa kuanza kufugwa na familia hiyo kuanzia
mwaka 1940 baada ya mamba mwingine aliyekuwa akifugwa kabla yake kuchukuliwa na
Wazungu.
Ajabu ni kwamba familia hiyo yenyewe huwa haiamini kwamba
ana nguvu zozote za kipekee.
Kiongozi wa sasa wa familia hiyo ya Delesolu, Bw Raufu
Yesufu, aliambia BBC kwamba: "Kwa sababu ya Imani yetu, sisi ni Waislamu,
hatuamini kwamba ana nguvu zozote."
Lakini hilo huwa haliwazuii watu kuendelea na imani zao.
No comments:
Post a Comment