KANISA Katoliki limesema mtawa Suzan
Bartholomew (48), aliyefariki dunia baada ya kujirusha chini kutoka
ghorofa ya pili ya moja ya majengo ya Hospitali ya Bugando, amezikwa kwa
heshima zote za kanisa kwa sababu alipata nafasi ya kutubu kabla umauti
haujamfika.
Mara baada ya taarifa za kujiua kwa
mtawa huyo kutolewa, mkanganyiko ulitokea ikiwa ni je atazikwa kwenye
makaburi ya watawa ama laa kwani katika imani ya dini yake, mtu
aliyejiua hukosa baadhi ya huduma wakati wa maziko yake.
Suzan ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Fedha
na Mipango wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa Bugando (BMC),
anadaiwa kujirusha ghorofani usiku wa kuamkia Agosti 27,2018.
Alilazwa wodi ya wagonjwa wanaohitaji
uangalizi maalumu (ICU) na kuendelea kupatiwa matibabu, lakini alifariki
dunia usiku wa Agosti 28, wakati akiendelea kutibiwa.
Inadaiwa alichukua uamuzi wa kujirusha
ili kujiua kutokana na sakata la upotevu wa Sh milioni 380 ndani ya
kipindi cha miezi miwili katika idara ya uhasibu ndani ya kitengo chake.
Kutokana na sakata hilo, maofisa kadhaa
walisimamishwa kazi, huku yeye akikamatwa na Jeshi la Polisi kuhojiwa na
kuachiwa kwa dhamana.
Jana, Padri Deodadus Kagashe alisema
Suzan alizikwa jana asubuhi katika makaburi hayo ili kutoa nafasi ya
kuendelea na maandalizi ya mapokezi ya mwili wa Askofu Nestor Timanywa
aliyefariki dunia mwishoni mwa wiki.
Akielezea sababu za kupata huduma za
misa, mmoja wa watawa wa Shirika la Theresia ambaye hakupenda kuandikwa
jina lake gazetini, alisema Suzan alipatiwa huduma zote za misa wakati
wa maziko yake kutokana na kupata wasaa wa kutubu kabla ya kufariki
dunia.
“Ni kweli hakuna misa kwa watu wanaojiua
bila ya kujali wadhifa wao, huyu alijirusha, hakufa papo hapo,
alichukuliwa na kukimbizwa theater (chumba cha upasuaji), alitibiwa
kutokana na kupata tatizo la spine code (uti wa mgongo), baada ya kupata
nafuu na kujitambua aliomba huduma ya kanisa na kutubu,” alisema mtawa
huyo.
Alisema japokuwa hawawezi kujua alitubu
nini, lakini baada ya kitendo cha kujaribu kujiua kwa kujirusha kukwama,
alichukuliwa akiwa hai, hivyo wakati akipatiwa matibabu aliomba kutubu
na kupatiwa mpako wa wagonjwa, hivyo alifariki kikristu.
Alisema amezikwa kikristo na kupata
huduma zote, kutokana na kutubu na kubainisha kuwa vinginevyo angezikwa
kawaida kutokana na misimamo na misingi ya kanisa kwa watu wanaojiua
kutopatiwa huduma ya misa.
“Juzi alfajiri tulimuaga Suzan kwa ibada
ya misa na jana tumemzika, unajua watu wengi walitaka kujua atazikwaje
kutokana na msimamo wa kanisa kutowafanyia ibada waumini au watawa
wanaofariki kwa kujiua, lakini kifo cha huyu ni tofauti kwani alipata
nafasi ya kutubu kabla ya kifo, hivyo amezikwa kwa heshima zote sawa na
Wakristo wengine,” alisema.
Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Rufaa ya
Kanda ya Bugando (BMC), Lucy Mogela, alisema mtawa huyo aliagwa kabla ya
kusafirishwa kwenda Bukoba kwa misa iliyofanyika katika Kanisa la
Bugando, lakini hakutaka kufafanua zaidi kwa madai kuwa utaratibu wote
na masuala mengine yatatolewa na mkuu wa shirika lake.
Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi wa
Idara ya Habari ya Jimbo Kuu la Mwanza, Padri Titus Ngapemba, alisema
suala kuhusu taratibu na ibada ya mtawa Suzan linapaswa kutolewa
ufafanuzi na Mkuu wa Shirika la Theresia aliyeko Bukoba.
Alipoulizwa iwapo Suzan alistahili
kupata misa ya kumuaga na ile ya maziko, alisema ni kweli katika
utaratibu wa Kanisa Katoliki huduma ya misa kwa mtu aliyejiua haitolewi
na kueleza kuwa utaratibu wa mtawa huyo ulikuwa tofauti kwani maelezo
aliyopata alitubu kabla ya kifo.
“Naomba nisiingie ndani, hayo
unayoniuliza nadhani ukiwasiliana na Mkuu wa Shirika la Theresia utapata
ufafanuzi, ninaweza kukueleza kwa ufupi kuwa mtu yeyote akifariki moja
kwa moja kwa kujiua ni kweli hapati huduma, sasa hii ni tofauti na
Sister Suzan, alijirusha hakufa papo hapo, hivyo naambiwa alipata wasaa
wa kutubu, hivyo alizikwa kwa heshima zote za kikristo, mengine
mtafuteni msimamizi wa shirika lake utaelezwa zaidi,” alisema.
Hata hivyo, Mkuu wa Shirika la mtawa
huyo la Mt. Therisia, Hyasinta Misingo, hakupatikana kutokana na kudaiwa
yupo kwenye majukumu mengine ya mapokezi ya mwili wa Askofu Timanywa.
Kwa upande wake, Askofu Msaidizi wa
Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini, alisema kwa sasa hawezi kuzungumzia
suala hilo kwani alikuwa kwenye msafara wa mazishi ya Askofu Timanywa na
kuahidi kulitolea ufafanuzi zaidi leo iwapo bado utahitajika.
“Sasa hivi nipo kwenye msafara wa
mapokezi ya mwili wa Askofu Timanywa, niulize ya askofu, hayo ya Suzan
kesho nitapata wasaa wa kuyazungumzia,” alisema Askofu Kilaini.
No comments:
Post a Comment