Watu watatu wanaotuhumiwa kuwa majambazi
wamepigwa mawe hadi kufa na wananchi wa Kijiji cha Bubare Wilaya ya
Missenyi mkoani Kagera.
Watuhumiwa hao waliuawa baada ya
kuwekewa mtego kutokana na kuwapo taarifa za wao kutaka kuvamia nyumba
ya mmoja wa wakazi wa kijiji hicho kwa nia ya kupora fedha za mauzo ya
mifugo.
Baadhi ya viongozi wa Serikali ya kijiji
waliojaribu kuwazuia wananchi kuwashambulia watuhumiwa hao,
walilazimika kutimua mbio kuokoa maisha yao baada ya kugeuziwa kibao na
kuanza kushambuliwa.
Mkuu wa Wilaya ya Missenyi, Denis Mwila
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwataka wananchi kuacha
kujichukulia sheria mikononi wanapowakamata watuhumiwa, badala yake
wawafikishe kwenye mikono ya vyombo vya dola kwa hatua za kisheria.
Akizungumzia namna njama za watuhumiwa
hao zilivyojulikana na kuwanasa, Mkuu huyo wa wilaya alisema uongozi wa
kijiji na jeshi la polisi walipata taarifa kutoka kwa raia wema kuhusu
watu kutaka kuvamia nyumba ya mkazi huyo aliyeuza mifugo yake Mei 16.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi alisema uchunguzi
kuhusu tukio hilo unaendelea na kuahidi kutoa taarifa baadaye.
No comments:
Post a Comment