Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini TFDA
limeendesha kikao kazi cha wahariri na waandishi wa habari mikoa ya
Shinyanga na Mwanza kwa ajili ya kuwashirikisha na kuhamasisha kazi na
majukumu ya TFDA na kujadiliana kwa pamoja namna ya kupambana katika
kuhakikisha kuwa soko la Tanzania lina bidhaa bora,salama na fanisi ili
kumlinda mlaji.
Kikao kazi hicho kimefanyika leo
Jumatatu Mei 21,2018 katika ukumbi wa mikutano wa TFDA Kanda ya ziwa
uliopo Buzuruga jijini Mwanza ambapo mgeni rasmi alikuwa mkuu wa mkoa wa
Mwanza,mheshimiwa John Mongella.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu TFDA, Bi.Agnes Kijo alisema kikao hicho kinahusu uhamasishaji wa sheria ya chakula, dawa na vipodozi.
Bi. Kijo alisema TFDA itaendelea
kufuatilia, kuondoa na kuteketeza bidhaa ambazo hazikidhi vigenzo vya
ubora, usalama na ufanisi ili kuepusha bidhaa husika kutumika ambapo
amewahimiza washiriki kufikisha elimu watakayoipata kwa wananchi.
Alisema TFDA imeendelea kutoa elimu kwa
wadau mbalimbali kuhusu usalama, ubora, ufanisi wa vyakula, dawa,
vipodozi, vifaa tiba pamoja na vitendanishi ili kusaidia kuondokana na
matumizi ya dawa na vyakula vyenye madhara.
Aliongeza kuwa hatua hiyo imesaidia TFDA
kutekeleza vyema majukumu yake ambapo kwa mwaka 2015/17 usajili wa
bidhaa umeongezeka kutoka bidhaa 7,010 hadi kufikia 9,180 hii ikiwa ni
ishara njema ya kuwepo ongezeko la uelewa wa matakwa ya sheria miongoni
mwa wafanyabiashara.
Akifungua kikao hicho,Mongella
alivipongeza vyombo vya habari,wahariri na waandishi wa habari ambao
wamekuwa wakitoa taarifa mbalimbali kuhusu umuhimu wa kudhibiti bidhaa
unaofanywa na na TFDA na hivyo kuongeza uelewa kwa jamii.
Baadhi ya wanahabari walioshiriki kikao
hicho wamesema bado kuna changamoto ya bidhaa zenye viambata sumu
kuingia sokoni hivyo watatumia vyema vyombo vyao vya habari kufikisha
elimu kwa jamii ili kujiepusha na matumizi ya bidhaa hizo.
No comments:
Post a Comment