Serikali imesema tangu kuanza kwa
matumizi ya sheria ya makosa ya mtandao namba 14 ya mwaka 2015,
imesaidia kupunguza makosa ya mtandao na upatikanaji wa haki pale mtu
anapotenda kosa tofauti na awali hivyo hawana mpango wowote kwa sasa
kufanya marekebisho kwenye sheria hiyo.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mei 21, 2018
na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa
Bungeni Jijini Dodoma kwenye kikao cha 33 mkutano wa 11 wa Bunge la 11
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati akijibu la nyongeza la Mbunge
wa Ubungo Said Kubenea aliyetaka kujua lini serikali itapeleka bungeni
mswada wa marekebisho ya sheria mtandao inayobana uhuru wa mwananchi
kupata habari.
"Uwepo wa sheria ya makosa ya mtandao
Na. 14 ya mwaka 2015 umesaidia kupungua kwa makosa ya kimtandao,
upatikanaji wa haki pale mtu anapotenda kosa kwani kabla ya hapo
kulikuwepo na changamoto na uanishaji wa makosa na adhabu hali
iliyopelekea haki kutopatikana", amesema Kwandikwa.
Pamoja na hayo, Kwandikwa ameendelea kwa kusema "uwepo
wa sheria hiyo umewezesha kuimarika kwa matumizi salama ya mtandao na
kuleta maendeleo kwa wananchi. Sheria hii ni muhimu sana kwa nchi yetu
na badala ya kuwaathiri watumiaji au wananchi imesaidia kupunguza
waharifu wa mtandao.....
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na
Jeshi la Polisi inaonyesha kupungua kwa makosa hayo kwa asilimia 48.9
kati ya Januari hadi Disemba 2017. Hivyo kwa sasa serikali haina mpango
wa kupeleka marekebisho ya sheria hiyo bungeni hadi hapo kutakapokuwa na
uhitaji wa kufanya hivyo".
Kwa upande mwingine, Kwandikwa amewataka
wananchi kutumia fursa chanya zitokanazo na matumizi sahihi ya mitandao
kuliko kutumia mitandao hiyo kuvunja sheria za nchi na maadili pamoja
na tamaduni za kitanzania.
No comments:
Post a Comment