Serikali ya Tanzania imezindua Mpango Mkakati wa nne wa Virusi vya Ukimwi ‘VVU’ na Ukimwi katika sekta ya afya kwa ajili ya mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi hususani katika makundi ya watu walio katika hatari ya kupata maambukizi.
Uzinduzi huo umefanyika leo Jumatano Mei
9,2018 katika ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Nyerere uliopo katika Chuo
cha Mipango Jijini Dodoma ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mheshimiwa Ummy Mwalimu.
Uzinduzi huo ulioambatana na sherehe za
kutimiza miaka 30 ya Mpango wa taifa wa kudhibiti Ukimwi (NACP)
umehudhuriwa na wadau mbalimbali wa afya yakiwemo mashirika ya kitaifa
na kimataifa yanayojihusisha ma mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi nchini
likiwemo shirika la AGPAHI.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango
Waziri Ummy Mwalimu alisema mpango huo unaweka msisitizo katika kutoa
huduma rafiki kwa vijana na makundi mengine katika jamii yaliyopo katika
hatari ya kupata maambukizi ya VVU hasa wanaotumia dawa za kulevya,
madereva wa magari ya masafa marefu, wavuvi na wafungwa.
“Mpango huu pia unaweka kipaumbele
katika kuboresha huduma za kinga, tiba na matunzo sambamba na kuweka
mazingira wezeshi ya kupata huduma hizo na kusisitiza na kuelekeza
kuimarisha uratibu na ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi
katika kutoa huduma za VVU na Ukimwi kwa watu waliopo katika wanaoishi
na VVU”,alieleza.
Hata hivyo, aliyapongeza mashirika na
taasisi mbalimbali zinazoendelea kushirikiana na serikali katika
mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi kwani Tanzania ya viwanda haiwezi
kuwepo kama wananchi hawana afya bora.
“Wizara yangu imekuwa ikishirikiana
na wadau wa kitaifa na kimataifa kuchukua hatua mbalimbali za
kuhakikisha Ukimwi unatokomezwa nchini na juhudi hizi zimekuwa zikilenga
kuzuia maambukizi mapya ya VVU na kutoa huduma za tiba na matunzo kwa
watu wanaoishi na VVU”,alisema.
“Tumeweza kupunguza maambukizi ya VVU
kitaifa kutoka asilimia 7 mwaka 2003/2004 na sasa hivi tumefikia
asilimia 4.7 kwa takwimu za mwaka 2016/2017”,alifafanua Waziri Ummy.
Alibainisha kuwa wakati maambukizi ya
VVU yakipungua kitaifa katika mikoa 11 hali ya maambukizi yamepanda
mfano; Tanga ilikuwa na maambukizi kwa asilimia 2.4% lakini sasa ni 5%,
Dodoma ilikuwa na 2.9% sasa ni 5% na Mwanza 4.2% sasa imekuwa 7.2 %.
Aidha alisema maambukizi ya VVU
yanaendelea kuwepo kutokana na wananchi wengi hususani wanaume
kutojitokeza kupima afya zao hivyo ipo haja ya kuangalia namna ya
kuwafikia watu hao.
“Changamoto kubwa ninayoiona sio
watanzania wengi kupata maambukizi ya VVU bali ni watanzania wenye
maambukizi ya VVU kutofahamu hali zao, kwani takwimu zinaonesha 48% ya
Watanzania wanaohisiwa kuwa na maambukizi ya VVU hawajui hali zao,
tunachopaswa ni kuwafikia watu hawa ili tuwaingize katika programu za
uanzishwaji na matumizi ya dawa za kupungua makali ya VVU (ART)",alisema.
Waziri Ummy alisema katika bajeti ijayo
serikali imepanga shilingi bilioni 5.5 kwa ajili ya kununua dawa za
magonjwa nyemelezi ili kuboresha huduma za afya katika vituo vya tiba na
matunzo nchini.
Waziri Ummy pia aliagiza kuanzia Julai
1, 2018 dawa zinazotolewa kwa watu wanaoishi na VVU zianze kutolewa kila
baada ya miezi mitatu badala ya kila baada ya miezi ilivyo sasa.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la
Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI), Dkt. Sekela
Mwakyusa aliishukuru serikali kwa kupanga bajeti ya shilingi bilioni 5.5
kwa ajili ya kununua dawa za magonjwa nyemelezi kwani miongoni mwa
changamoto kubwa katika vituo vya tiba na matunzo ni uhaba wa dawa hizo.
“Nimshukuru sana mheshimiwa Ummy
Mwalimu kwa kutoa agizo la dawa za watu wanaoishi na maambukizi ya VVU
kupewa kila baada ya miezi mitatu, hii itapunguza mzigo wa wagonjwa
kwenye vituo kwa sababu tumekuwa tukikabiliwa na changamoto hii kwenye
vituo vya tiba na matunzo”,alisema.
Alisema kitendo cha kutoa dawa kila
baada ya miezi mitatu mbali na kusaidia kupunguza mzigo wa wagonjwa, pia
watoa huduma watafanya kazi zingine na kuepusha usumbufu kwa wateja
waliopo katika huduma.
Aliongeza kuwa ili kuwafikia Watanzania
waliopo katika 48% ambao hawafahamu hali zao kiafya,shirika la AGPAHI
linaendelea na mikakati ya kuyafikia makundi maalumu.
“Sisi kama wadau wa mapambano dhidi
ya VVU na Ukimwi, tunaendelea na jitihada za kuwapata wateja kwa
kuyafikia makundi yanayotakiwa, ikiwa ni pamoja na kuwapima watoto wa
wateja na kuhakikisha vituo vya afya vinakuwa rafiki kwa wanaume ikiwemo
kuongeza muda wa kliniki”,alieleza Dkt. Sekela
No comments:
Post a Comment