SERIKALI ya Tanzania imetiliana saini na Serikali ya
China mkataba wa msaada wa kiasi cha Shilingi Bilioni 146.47. Mkataba
huo umesainiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dotto James na
Balozi wa China nchini Wang Ke Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo Katibu Mkuu alisema kuwa
fedha hizo ni msaada na siyo mkopo na zitatumika katika miradi miwili ya
miundombinu. Mradi wa kwanza ni ujenzi wa Chuo Kikuu cha Usafirishaji
cha Taifa (NIT) ambacho kitajengwa Mabibo Jijini Dar es Salaam kwa
gharama ya Dola za Marekani milioni 62 sawa na takriban Shilingi bilioni
138.3.
Mradi wa pili ni kwa ajili ya kusaidia upembuzi yakinifu na upembuzi
sanifu wa mradi wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa
(SGR), ambapo kiasi cha Sh. bilioni 3.2 kimetengwa kwa ajili hiyo.
Bw. Doto James alisema kwa sasa mradi wa ujenzi wa reli ya kati kwa
kiwango cha Kimataifa umeanza kwa awamu mbili ambazo moja ni kuanzia Dar
es Salaam hadi Morogoro, na kuanzia Morogoro hadi Makutopora-Dodoma,
upembuzi yakinifu utakaofanywa na Serikali ya China ni kwa maeneo
mengine ya ujenzi wa Reli hiyo kuanzia Dodoma, Tabora hadi Mwanza na
Kuanzia Kaliua hadi Kigoma.
“China imetusaidia miradi mingi ikiwemo mradi wa maji Chalinze,
Ujenzi wa uwanja wa Michezo wa Taifa, Mradi wa teknolojia za Kilimo
mkoani Morogoro, Kituo cha upasuaji wa moyo na mafunzo, Kituo cha
Mikutano cha Kimataifa cha Nyerere pamoja na misaada ya dawa na vifaa
tiba” alieleza Bw. James
Kwa upande wake Balozi wa China hapa nchini, Wang Ke, Alisema kuwa
China inategemea kuona kuwa msaada huo utasaidia kuimarisha maendeleo na
kuisaidia Tanzania kupata maendeleo haraka.
Aidha alisema China itaendelea kushirikiana na Tanzania katika
kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo ambayo itawasaidia
Watanzania na kuendeleza urafiki uliopo kati ya nchi hizi mbili.
Balozi Wang Ke, amesema Pia Serikali ya China na Tanzania zinaendelea
majadiliano kuhusu ujenzi wa bandari ya Bagamoyo, na kuongeza kuwa
majadiliano hayo yatakapokamilika nchi yake itasaidia ujenzi wa bandari
hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Usafirishaji Taifa (NIT) Prof.
Zacharia Mganilwa ameishukuru Serikali ya China kwa msaada huo na kusema
kuwa msaada huo utaisaidia chuo hicho kuweza kutoa wataalamu wa kutosha
kuweza kushiriki katika ujenzi wa miundombinu ikiwemo sekta ya anga.
Amebainisha kuwa Chuo hicho Kikuu kitatoa mafunzo kwenye fani muhimu
na zinazohitajika ikiwemo ufundi wa reli, masuala ya anga na sekta
nyingine mtambuka kwa kutoa wataalamu waliobobea watakao changia
kufanikisha azma ya Serikali ya uchumi wa viwanda.
Kwa upande wake Kaimu Naibu Mkurugenzi Uendeshaji wa Shirika la Reli
Tanzania-TRC, Bw. Focus Msasani ameeleza kuwa msaada huo wa shilingi
bilioni 3.22, utasaidia kuipunguzi serikali gharama ilizokuwa izitumie
kwa kazi hiyo kenye mradi mkubwa wa kihistoria wa ujenzi wa Reli ya Kati
kwa kiwango cha Kimataifa.
No comments:
Post a Comment