Mtoto wa miezi miwili jina limehifadhiwa
mkazi wa Kitongoji cha Unyanyembe kata ya Kizumbi manispaa ya
Shinyanga amenusurika kufa baada ya kunyeshwa sumu ya panya na baba
yake mzazi Edson Timotheo Damiani (37) kwa kile kilichoelezwa ni kutaka
kuficha siri ili mkewe asijue kama amezaa mtoto mwingine nje ya ndoa.
Akielezea tukio leo Aprili 12,2018 Mama
mzazi wa mtoto huyo Maria Shija amesema lilitokea Mach 24 mwaka huu
majira ya saa tatu usiku ambapo baba wa mtoto huyo alikwenda nyumbani
kwa mwanamke huyo kwa ajili ya kumsalimia mtoto wake ndipo akamnywesha
sumu ya panya kwa lengo la kumuua.
Amesema wakati kitendo hicho kikifanywa
na mzazi mwenzake huyo alikuwa akimtuma maji ya kunywa mara kwa mara
ambapo siyo kawaida yake na aliporudisha kikombe ndani ndipo akasikia
harufu ya dawa ya panya na aliporudi kwa mtoto haraka akamkuta ameanza
kutoa mapovu na mwanaume kukimbia na kopo la sumu ya panya.
“Nilipobaini kuwa mtoto kapewa sumu
nikakimbia kwa jirani anayefuga ng’ombe, ndipo nikachukua maziwa
nikamnywesha, na baadae nikachukua bodaboda hadi kituo cha polisi kupewa
RB na kisha kwenda hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga kupatiwa
matibabu, na sasa mtoto wangu ni mzima”,amesema Shija.
"Mwanaume huyu ni katibu wa CCM kata ya Kitangili manispaa
ya Shinyanga na wakati ananitongoza aliniambia hana mke na baada ya
kuzaa huyu mtoto ndipo akasema ana mke na hamtaki kwani atavunja ndoa
yake, na ndiyo chanzo cha kutaka kumuua kwa kumywesha sumu ya panya”,aliongeza.
Naye mtu wa karibu na familia hiyo
Jumanne Kagusa, amesema baada ya kuona mtuhumiwa huyo anazagaa mitaani
na kutochukuliwa hatua yoyote ya kisheria ndipo naye akafika kufuatilia
suala hilo kwa jeshi la polisi na hatimaye juzi akakamatwa na kuswekwa
rumannde.
Kwa upande wake kamanda wa jeshi la
Polisi mkoani Shinyanga Kamishina msaidizi wa Polisi Simon Haule
amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na mtuhumiwa anashikliwa na
kubainisha kuwa upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani kujibu
shitaka linalomkabili.
No comments:
Post a Comment