Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Tanzania (KKKT), Dk. Fredrick Shoo, amesema wale wote wanaojaribu
kupotosha ukweli wa waraka wa maskofu kwa kuupaka matope ni wajinga.
Askofu Shoo ametoa kauli hiyo leo katika
Usharika wa Moshi Mjini Dayosisi ya kaskazini, mkoani Kilimanjaro
wakati akitoa salamu za Pasaka katika ibada maalumu ya kusherekea
sikukuu hiyo.
Amesema kumekuwa na baadhi ya watu
wakiwamo wanasiasa ambao wamekuwa wakitumia nguvu nyingi kupotosha
waraka wa maaskofu hao na kulipaka kanisa matope kwa malengo yao
binafsi jambo ambalo halipendezi na kwamba watu hao ni wajinga.
“Wapo wanaotumia nguvu nyingi kutaka
kupotosha ujumbe wa waraka wa maaskofu na wamekuwa wakilipaka kanisa
matope ili waweze kurejea katika waraka ule, watu hawa naweza kuwaita ni
wajinga lakini pamoja na hilo nataka wakayatafakari na kama wanaona
kuna hatua za kuchukua wachukue.
“Kanisa limekuwa linapata kejeli za aina
mbalimbali kutoka kwa watu hao na kuwatuhumu kuwa maskofu walifikia
maamuzi ya kuandika waraka huo kutokana na sababu za kimaslahi kwa maana
ya sadaka makanisani kupungua jambo ambalo si la kweli.
“Kanisa linasitikika sana, tunaposema
jambo la kweli na jambo linalohusu maisha ya Watanzania wote, halafu
kunatokea watu chache ambao naweza kuwaita wajinga wanakebehi na kusema
eti kwa sababu sadaka zimepungua kanisani sisi sadaka hazijapungua kwani
wakristo wanajitoa sana na hatujapungukiwa na kitu ila tunasema yale
tunayoyaamini,” amesema.
Askofu Shoo amesema anafahamu kuwa
kupitia waraka ule maaskofu wa kanisa hilo watabatizwa majina ya aina
mbalimbali na kwamba hizo ni jitihada za kujaribu kuuzima ukweli ulipo
katika wataka huo na wao hawajali kuhusu hilo bali watasimamia ukweli
zaidi.
“Najua tutaitwa majina mengi maaskofu na
hizo ni jitihada za upotoshaji wa ule ukweli ulipo katika waraka na
tukumbuke hili si jambo la hivi hivi tu…. kwani kwa wakati mmoja
mabaraza ya maaskofu wa makinsa makubwa mawili nchini kukaa na kutoa
waraka ambao una ujumbe ulioshabihiana si kitu cha kawaida mimi nasema
kuna kitu Mungu anataka kutuambia kupitia ujumbe ule tutafakari hili
kama taifa,” amesema.
No comments:
Post a Comment