Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la
Tanga, Mhashamu Anthony Banzi ameitaka jamii kuiheshimu miili ya
marehemu kwa kuwapa maziko ya heshima badala ya kuwafunga kwenye viroba
na kuwatupa kwenye maji.
Amesema jambo ambalo si zuri machoni kwa
wanadamu na kwa Mwenyezi Mungu na pia inakiuka utamaduni wetu kama
Watanzania ambapo ameitaka jamii kubadilika kwa vitendo vya namna kwani
vinaondoa utu wao.
Ameyasema hayo leo Jumapili Aprili Mosi,
wakati akitoa salamu za Pasaka kwa waumini wa kanisa hilo kwenye misa
iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Anthony wa Padua, Chumbageni
Jijini Tanga.
“Lazima tuwaheshimu marehemu katika nchi
yetu, pengine tunataka kuwa na utamaduni tofauti wafu wengi tunaambiwa
wameokotwa ndani ya viroba kwenye maji na kuzikwa, je hali hii
inatupeleka wapi kama taifa” Tujitafakari kwa jambo hilo.
“Kama unavyoheshimika ukiwa mzima,
marehemu pia wanapaswa kuheshimika hata wanapokuwa wamefariki kwa
kuhifadhiwa mahali ambapo hawawezi kuonekana tena,” amesema.
Aidha, amewataka viongozi ambao
wanajukumu la kulinda usalama wa nchi, kuhakikisha wananchi wanaishi kwa
amani na utulivu ambayo ni tunu tulioachiwa na waasisi wa taifa hili.
“Mara nyingi tumesikia raia wema wametoa
taarifa ya kukamatwa wahalifu hivyo ni jukumu la waliochaguliwa
kutazama usalama wao kwa lengo la kuwawezesha kutimiza majukumu mengine
ya kimaendeleo,” amesema Askofu Banzi.
No comments:
Post a Comment