Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu
Mkoani Manyara, imepokea kutoka serikali kuu kiasi cha sh1 bilioni kwa
ajili ya ujenzi wa makao makuu mapya yatakayojengwa Mji mdogo wa
Haydom.
Pia, kwenye bajeti ya mwaka wa
fedha wa 2018/2019 Halmashauri hiyo imetengewa sh. 2.3 bilioni za ujenzi
wa jengo la ofisi na nyumba za kuishi watumishi.
Mkurugenzi mtendaji wa
halmashauri hiyo Hudson Kamoga aliyasema hayo jana wakati akizungumza
juu ya mikakati ya ujenzi wa makao makuu mapya yatakayojengwa Haydom.
Alisema baada ya kikao cha
kamati ya ushauri ya mkoa huo kupitisha uamuzi wa ujenzi wa makao makuu
ya halmashauri hiyo kuwa Haydom, hivi sasa wapo kwenye mchakato wa
utekelezaji.
“Hadi mwakani kipindi kama hiki
tutakuwa tumeshahamia kwenye makao makuu mapya ya halmashauri yetu kule
Haydom na kuondoka hapa Mbulu mjini,” alisema Kamoga.
Alisema awali Mbulu iligawanywa
mwaka 2015 na kuwa na halmashauri mbili ya mji na wilaya, hivyo huu ni
wakati wa kujenga ofisi zao mpya kwa lengo la kusogeza huduma za jamii
karibu na wananchi.
“Tunaishukuru serikali
inayoongozwa na Rais John Magufuli kwa kutupatia fedha hizo za ujenzi
wa makao makuu mapya ya halmashauri yetu ya wilaya,” alisema Kamoga.
Mkazi wa mji mdogo wa Haydom,
Paul John alishukuru uamuzi wa kujengwa makao makuu mapya kwenye eneo
hilo tofauti na uamuzi wa awali wa kujenga Dongobesh.
“Huku kuna huduma mbalimbali za
kijamii nyingi ikiwemo kituo kikubwa cha polisi, benki hospitali kubwa,
tofauti na Dongobesh ambayo haina hata benki,” alisema John.
Mkazi wa Dongobesh Aloyce Martin
alisema kuenea kwa unywaji na biashara ya pombe haramu ya gongo kwenye
eneo hilo kumewagharimu hadi kusababisha makao makuu mapya ya
halmashauri hiyo yakahamishiwa Haydom.
“Makosa ni ya kwetu sisi wenyewe
kwani tulipata nafasi badala ya kuitumia ipasavyo sisi tukaichezea hadi
ikawadondokea watu wa Haydom,” alisema Martin.
No comments:
Post a Comment