Watoto 67 wilayani Tarime mkoani Mara
wamekataliwa na familia zao baada ya kukataa kukeketwa na kukimbilia
kwenye kituo cha kuhifadhi wasichana wanaokataa kutekeleza mila hiyo.
Watoto hao wametua na kupokewa na kituo
cha Association For Termination of Female Genital Multilation (ATFGM
Masanga) kilichopo mjini hapa. Kufuatia hatua hiyo, Serikali imewataka
wazazi hao kutoa malezo ya kuwakataa watoto wao baada ya kukataa
kufanyiwa unyama huo kabla hawajachukuliwa hatua za kisheria.
Akitoa agizo hilo kwa niaba ya mkuu wa
Wilaya ya Tarime, Glorious Luoga, kaimu ofisa elimu msingi wa
halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Amos Waitara alivitaka vyombo husika
vya Serikali kuhakikisha watoto hao wanapata haki za malezi kutoka kwa
wazazi wao.
Waitara alitoa agizo hilo wakati wa
kufunga kambi ya wasichana 103 waliokuwa wamekimbilia katika kituo hicho
na kupewa mafunzo mbadala dhidi ya madhara ya ukeketaji na tohara.
“Hatuwezi kulifumbia macho suala hili
kwa baadhi ya wazazi hawa kuminya uhuru wa watoto walioona mbali na
kuchukua jukumu la kupinga vitendo vya kikatili vya ukeketaji, wazazi
hao waitwe na kueleza kwa maandishi sababu za kuwanyanyasa,” alisema .
Meneja miradi ATFGM, Valerian Mgani
alisema tangu kituo hicho kilipoanzishwa mwaka 2008 wamekuwa wakipokea
watoto ambao wanakimbia ukeketaji.
Wasichana hao hutoka wilaya za
Serengeti, Tarime, Loliondo na nchi jirani ya Kenya na kambi
inapomalizika hurudishwa nyumbani na baadhi yao wamekuwa wakikataliwa na
wazazi.
Naomi Baraka kutoka nchi jirani ya Kenya
ambaye alishiriki mafunzo hayo ya tohara mbadala, aliiomba Serikali ya
Kenya kuthamini watoto wa kike huku akiitaka jamii kuondokana na mila
ambazo zimepitwa na wakati.
Baadhi ya mabinti ambao hawakutaka
kutaja majina yao kutoka kata za Sirari, Pemba na Nyanungu wilayani
Tarime waliolazimishwa kuolewa katika umri mdogo na kukimbilia kituoni
hapo waliiomba Serikali kuingilia kati jambo hilo. Kituo cha ATFGM
Masanga mpaka sasa kina mabinti 2,572.
No comments:
Post a Comment