Wakati uongozi wa kata ya Nyehunge wilayani Sengerema ukipitisha sheria
ya kuwacharaza viboko 12 au faini ya Sh10,000 wanaume watakaokutwa
wamesimama na wanafunzi wa kike, Wilaya ya Tandahimba imekamata
wanafunzi watano waliopata ujauzito mwaka jana.
Sheria hiyo ndogo imepitishwa juzi kwenye kikao cha maendeleo ya kata
(WODC) baada ya tatizo la wanafunzi kukatisha masomo kutokana na kupata
uja uzito kuzidi kuwa sugu.
Ofisa mtendaji wa Kata ya Nyehunge, Mabula Enock alisema sheria hiyo
itasaidia kudhibiti vitendo vya wanaume wanaoshawishi wasichana kufanya
nao mapenzi na baadaye kuwapa ujauzito unaokatisha ndoto zao.
“Tumelazimika kupitisha sheria hiyo ili kuungana na mkuu wa wilaya yetu,
Emmanuel Kipole aliyeagiza wanaume watakaokutwa wamesimama na wanafunzi
wacharazwe viboko au kutozwa faini ya Sh10, 000 ama vyote kwa pamoja,”
alisema Enock.
Agizo la mkuu huyo wa wilaya alilitoa Oktoba mwaka 2017 wakati
akikaribisha wanafunzi 81 kujiunga na masomo ya kidato cha tano katika
Shule ya Sekondari ya Nyehunge.
Mkazi wa kata hiyo, Mussa Kazimili alisema sheria hiyo ndogo itasaidia
kupunguza tatizo hilo na kuwataka wananchi na wazazi kusaidia kubaini
wanaume watakogundulika kufanya vitendo hivyo.
Diwani wa kata hiyo, Charles Mbogo alisema kitendo cha kukatiza masomo
si cha kuungwa mkono, hivyo adhabu inapaswa kuongezwa na kuitaka jamii
kuachana na suala hilo.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na ofisa elimu ya sekondari wa
Buchosa, Benjamini Siperato halmashauri hiyo ina jumla ya wanafunzi
1,136 katika shule 20 za sekondari 20 na mwaka 2016/17 wanafunzi 18 wa
kike walipata ujauzito, hivyo jamii inapaswa kuacha tabia ya kuwarubuni
watoto wa kike.
Wakati huohuo, serikali wilayani Tandahimba imewakamata wanafunzi watano
waliopata ujauzito kwa lengo la kutaka habari kuhusu wanaume waliowapa
ujauzito na kukatiza masomo yao.
Katibu tawala wa wilaya hiyo, Mohamed Azizi, ambaye alikuwa akizungumza
kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Tandahimba, Sebastian Waryuba, alisema
wanafunzi ha walikamatwa na watoto wao, lakini wahusika hawajakamatwa.
“Tumefanikiwa kuwakamata wazazi na wanafunzi watano wakiwa wamejifungua.
Kati yao, mmoja aliacha shule akiwa kidato cha nne,” alisema.
“Wengine watatu wa kidato cha pili. Baada ya kuzungumza nao wamesema
hawapati huduma zozote kutoka kwa wahusika ambao wamewapa ujauzito. Hali
hiyo ni wazi kuwa inawapa shida wazazi.”
Alisema wazazi wamekuwa wakilaumiwa kwa kushindwa kutekeleza majukumu
yao ipasavyo ili kuhakikisha watoto wao wanamaliza elimu ya sekondari
bila kupata ujauzito.
“Inasikitisha. Mmoja ameacha shule akiwa kidato cha nne mwaka jana,
alibakiza siku chache tu aweze kumaliza masomo yake. Hili liwe somo kwa
wazazi na wanafunzi wengine.
No comments:
Post a Comment