Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imemuibukia kivingine, Askofu wa
Kanisa la Full Gosper Bible Fellowship (FGBF), Zakaria Kakobe, kuhusu
utajiri alionao ikisema haina muda wa kulumbana naye, bali inatekeleza
maelekezo ya Kamishna Mkuu.
Aidha, mamlaka hiyo imesema haitaki kuwa kwenye malumbano na askofu huyo
wakati ikiendelea na uchunguzi dhidi ya vitega uchumi vyake na
kuangalia kama analipa kodi ya serikali.
Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, jana alisema
maofisa wao wanaendelea kutekeleza tamko la Kamishna Mkuu wa TRA,
Charles Kichere, la kuchunguza utajiri wa Askofu Kakobe.
"Sisi (TRA) hatutaki kuwa kwenye malumbano na Kakoke, tulichosema
tumeishia hapo. Alichosema Kamishna Mkuu tunaishia hapohapo, hatutakiwi
kujibishana naye," Kayombo alisema.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam
Jumamosi, Kichere alisema mamlaka yake imeipokea kwa furaha kauli ya
Askofu Kakobe kuhusu utajiri wake na inataka kujiridhisha vyanzo vya
utajiri huo.
Kichere alisema TRA inafahamu kuwa shughuli za kidini hazitozwi kodi,
lakini inataka kufahamu kama fedha hizo za Askofu Kakobe zinatokana na
sadaka pekee.
Alisema wameamua kuchukua uamuzi huo kutokana na kiongozi huyo wa kiroho kutokuwamo katika kumbukumbu za ulipaji kodi za TRA.
Kauli iliyoleta utata na kuibua uchunguzi huo ni ya Askofu Kakobe
kukaririwa wiki iliyopita akidai ana fedha nyingi kuliko serikali na
anao uwezo wa kumkopesha waziri pindi akiombwa kufanya hivyo.
Hata hivyo, juzi ikiwa ni siku moja baada ya TRA kutangaza kufanya
uchunguzi dhidi yake, Askofu Kakobe alieleza historia ya maisha yake,
mali za kanisa na zake na misukosuko aliyopitia na kusisitiza kuwa
tafsiri iliyofanyika dhidi ya kauli yake kuhusu utajiri ni ya kimwili na
siyo ya kiroho. Alidai kauli yake ilimaanisha yeye ni tajiri wa kiroho
na si fedha.
Askofu Kakobe aliishauri TRA kutohangaika naye, badala yake ikatafute
fedha mahali kwingine akieleza kuwa ana nyumba moja iliyopo Kijitonyama
jijini na aliijenga mwaka 1986 kwa gharama ya Sh. milioni mbili ikiwa ni
pamoja na gharama za kiwanja.
Huku akishangiliwa na waumini wa kanisa lake kwenye ibada ya kuuaga
mwaka 2017, Askofu Kakobe pia alidai kuwa mwaka 1995 alinunua gari aina
ya Nissan Patrol kwa kutumia sadaka za washirika wa kanisa na hivi
karibuni waliibuka watu waliochangishana na kumnunulia gari jingine.
Alidai kuwa hata kwao Kakonko, Kigoma hajawahi kujenga hata choo na
kilichopo ni makaburi ya wazazi wake waliozikwa kwenye eneo la kuingia
kwenye nyumba iliyojengwa na wazazi wao.
Askofu Kakobe pia alidai kuwa kanisa la FGBF ndani na nje ya nchi halina
mradi wowote wa kiuchumi kama shamba au hoteli na akasisitiza serikali
ichunguze kote huko.
Alibainisha kuwa makusanyo yote ya sadaka huhifadhiwa kwenye akaunti
iliyofunguliwa mwaka 1990 katika Benki ya NBC na ni mali ya bodi ya
wadhamini ambayo imesajiliwa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini
(Rita).
No comments:
Post a Comment