Rais wa Uganda Yoweri Museveni
ameidhinisha mswada unaoondoa kikomo cha umri kwa wagombea urais nchini
humo, hatua inayompa nafasi ya kuwania tena urais mwaka 2021.
Kwa kuwa sheria hiyo itaanza kutekelezwa sasa, Bw Museveni anaweza akaongoza taifa hilo hadi 2031.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor la Uganda, katibu wa rais Bi Linda Nabusayi amesema Bw Museveni alitia saini mswada huo kuwa sheria Desemba 27 na kisha akatuma waraka tarehe 29 Desemba.
Sheria ya awali ilikuwa inamzuia mgombea kuwania urais baada ya kutimiza umri wa miaka 75.
Bw Museveni kwa sasa ana miaka 73.
Hatua ya rais huyo kuidhinisha mswada huo imetoa wakati ambao amekuwa akihimizwa na viongozi wa kidini na wanaharakati wa kisiasa kutouidhinisha.
Bunge liliidhinishwa mswada huo mnamo tarehe 10 Desemba kwa zaidi ya theluthi mbili ya wabunge waliohudhuria kikao, wabunge 317 wakiunga mkono na 97 wakapinga.
Wakosoaji, kama Dkt Kizza Besigye, mgombea urais wa zamani, anasema wabunge 317 waliounga mkono muswada huo, upande mmoja walihamasishwa na uroho, na upande mwengine kutojua matokeo ya matendo.
Kinyume na hayo, Rais Museveni katika hotuba yake ya kukaribisha mwaka mpya aliwasifu wabunge hao 317 kwa kupuuza vitisho na chuki.
Alisema wabunge hao walitekeleza wajibu wa kihistoria.
Sasa muswada huo uliotiwa sahihi na Rais Museveni utachapishwa katika gazeti la serikali kabla ya kuwa sharia kamili.
Hata hivyo, tayari kuna makundi yanapanga kwenda mahakama ya Kikatiba kuipinga sheria hiyo.
Na vyama vya upinzani vinasema, kuanzia wiki ijayo, vinapanga kampeni dhidi ya kubadilishwa Katiba ya 1995 na kuondolewa kwa kikomo cha miaka kwa wagombea wa urais.
No comments:
Post a Comment