Mbunge wa Jimbo la Mbozi (Chadema), mkoani Songwe, Pascal Haonga, amejitabiria mabaya baada ya kuwataka wananchi kuchoma nyumba yake iwapo atahamia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Haonge amewataka wananchi hao kufanya
hivyo kutokana na baadhi ya viongozi wa upinzani hususan madiwani na
wabunge kujiuzulu na kuhama vyama vyao.
Idadi kubwa ya madiwani wa upinzani
wamejiuzulu na kuhama vyama vyao na kujiunga na CCM wakati wabunge
watatu hadi sasa wamejiuzulu na kuhama vyama vyao ambao ni Godwin Mollel
(Siha-Chadema) aliyehamia CCM, Lazaro Nyalandu (Singida Kaskazini-CCM)
aliyehamia Chadema na Maulid Mtulia (Kinondoni-CUF) aliyejiuzulu na
kujiunga na CCM.
Haonga alitoa maelekezo hayo Jumamosi
alipowahutubia wananchi wa Mji wa Mlowo wilayani Mbozi, ambapo alisema
hawezi kuwasaliti wananchi waliosimama kidete kipindi cha Uchaguzi Mkuu
wa 2015 kuhakikisha anapata ushindi.
Alisema wakati wa uchaguzi kulikuwa na
matukio ya vurugu katika jimbo hilo huku baadhi ya watu wakipoteza
biashara zao, kujeruhiwa na wengine waliwekwa ndani kwa ajili ya
kupigania ushindi wake na wa Chadema, hivyo hawezi kuwasailiti.
Aliwaponda baadhi ya wabunge na madiwani
wa chama hicho na vyama vingine vya upinzani wanaohamia CCM kwa madai
ya kuunga mkono Serikali ya awamu ya tano kuwa hawatumii akili bali
wanatumia matope.
“Najua baada ya baadhi ya wasio na
msimamo kuanza kuhamia CCM, mmepata hofu kuwa hata kwangu itakuwa hivyo,
niwahakikishie mimi siwezi kulamba matapishi yangu, kuna watu mlipigwa
mabomu ya machozi, kuna watu walifungwa na kuna wengine walijeruhiwa
kuhakikisha tunashinda, ikitokea hivyo kateketezeni nyumba yangu,”
alisema Haonga.
Aidha Mbunge huyo alisema kuna baadhi ya
viongozi wa CCM wanajinadi wanataka kulirejesha jimbo hilo mikononi
mwao na kwamba hawataweza kwa kuwa chama hicho hakiaminiki tena na
wananchi.
Alisema kwa sasa wanajipanga kuhakikisha
wanapata ushindi mkubwa kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwakani,
ili kujihakikishia ushindi zaidi kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Aidha, alisema anaendelea kuzitumia
fedha za Mfuko wa Jimbo kuboresha miundombinu zikiwamo zahanati, vyumba
vya madarasa kwenye shule za msingi na sekondari pamoja na barabara ili
kuwapunguzia wananchi mzigo wa kuchangia.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mafunzo Chadema
Kanda ya Nyasa, Mdude Nyagali, alisema madiwani na wabunge wanaohamia
CCM wakidai wanaunga mkono Serikali ya awamu ya tano ‘wananunuliwa’.
Alisema mbwembwe za viongozi wa CCM
katika Mkoa huo kutaka kurejesha majimbo yote ya upinzani kwenye
uchaguzi Mkuu wa 2020 ni ndoto na haitatokea.
Vilevile alisema baadhi ya viongozi na
wanachama wa CCM wanaodai Chadema kinaelekea kufa, watakufa wao na sio
chama hicho ambacho alidai kinakubalika kila eneo kwa sasa tofauti na
miaka iliyopita.
Alidai uchaguzi wowote kura za CCM
hazipo maeneo ya vijijini wala mjini bali zipo kwenye vyombo vya Dola
likiwemo Jeshi la Polisi.
“Watawezaje kurejesha majimbo yetu
wakati waliahidi milioni 50 kila kijiji, zahanati kila kijiji na
kuboresha miundombinu ya barabara ambayo mpaka sasa hawajatekeleza?”
Alihoji.
Diwani wa Kata ya Mlowo, Sebastian Kilindu, aliwataka wananchi wa kata hiyo kumkatakata mapanga endapo ‘atanunuliwa’ na CCM.
Alisema kwa sasa ana misukosuko mingi ya
kisiasa katika wilaya hiyo, hasa kwenye vikao vya Baraza la Madiwani
kwa madai baadhi ya viongozi wa Halmashauri wanaongoza kimabavu.
No comments:
Post a Comment