WAZIRI wa Katiba na Sheria, Profesa
Palamagamba Kabudi amewataka viongozi wa dini nchini kutimiza wajibu wao
na kuhakikisha wanahifadhi vyema mapato ya fedha na kuyaweka wazi kwa
waumini ili kuondokana na migogoro isiyokuwa ya lazima kwenye nyumba za
ibada.
Aliyasema hayo jana alipokuwa mgeni
rasmi kwa niaba ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika Kanisa la
Anglikana, Dayosisi ya Shinyanga kwenye ibada ya kumuweka wakfu na
kitini askofu wa pili wa dayosisi hiyo Johnson Chinyong’ole ambaye
alikuwa Katibu Mkuu wa Kanisa la Angilikana nchini kisha mwaka jana
kupendekezwa kuwa askofu.
Kabudi aliwataka viongozi wa dini
kutimiza wajibu wao na kuhakikisha wanahifadhi vizuri mapato ya fedha
kwa kuhakikisha yanaonekana kwa waumini ili kuondokana na migogoro
inayoibuliwa ndani ya nyumba za ibada ikihusishwa na vitendo vya rushwa
na ufisadi.
“Tunatambua Kanisa la Angilikana
limekuwa mstari wa mbele katika kutoa huduma za kijamii kama maji, elimu
na afya pale ambapo serikali imekwama kupafikia. Dayosisi hii ni yenu
wala siyo ya wazungu hivyo ni wajibu kwenu kuhakikisha mapato ya fedha
anaonekana ili kuondoa migogoro isiyokuwa ya lazima kati ya viongozi na
waumini,” alisema Waziri Kabudi.
Aliongeza: “Serikali haina dini lakini
ni wajibu wa kila Mtanzania kuwa na dini yake hivyo viongozi wa dini
wanatakiwa kuwa kiungo kati ya waumini na askofu ikiwa kuwakumbusha
kupiga vita rushwa, vitendo vya kishirikina na ufisadi ambao serikali ya
Rais Dk John Magufuli imekuwa ikipiga vita kila siku”.
Pia alitoa rai kwa askofu aliyewekwa
wakfu na kitini, Chinyong’ole kuwa awakumbushe waumini maadili ya kanisa
katika kuwajenga kiroho na kiuchumi lakini pia kutumia uongozi wake
kuwajenga waamini ili waweze kushirikiana kwenye mipango mbalimbali ya
maendeleo.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika ambaye
ni mlezi wa kanisa hilo alisema kuwa kanisa hilo limepitia wakati mgumu
kwani kulikuwa na vuguvugu la migogoro kwa baadhi ya waumini kujidai
wanazishika nyadhifa ambazo kuzipata zimeonekana kumbe kunautaratibu
wake hivyo kushikamana na kwa umoja na kuepuka migogoro.
Askofu Mkuu wa kanisa hilo nchini, Jacob
Chimeledya alisema kuwa kuna kazi kubwa na kwamba hali iliyopo ni
mapito hivyo aliiomba serikali kulisimamia kanisa hilo kiuchumi kwani
tayari limeanza mchakato wa kuanzisha chombo chake cha kusimamia na
kuliangalia mali zake.
No comments:
Post a Comment