Naibu Waziri wa Nishati, Subira
Mgalu amewataka wakandarasi wanaojenga miundombinu ya usambazaji wa
umeme vijijini chini ya Wakala wa Nishati Vijijini Awamu ya Tatu (REA
III) kuongeza kasi ili miradi yote iweze kukamilika ifikapo mwaka
2019.
Mgalu aliyasema hayo mapema leo
tarehe 15 Desemba, 2017 katika ziara yake aliyoifanya katika kijiji cha
Bwitini wilayani Korogwe mkoani Tanga, lengo likiwa ni kukagua hatua
ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini iliyopo chini ya REA Awamu
ya Tatu na kutorishishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Katika ziara hiyo Naibu Waziri
Mgalu aliambatana na watendaji kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la
Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Alisema kuwa, Serikali
ilikwishawalipa wakandarasi wote malipo ya awali na kuwataka kuanza
kazi mara moja lakini wamekuwa wakifanya katika kasi ndogo hususan
katika hatua ya upembuzi yakinifu.
“ Wakandarasi wengi wamekuwa
wakichukua muda mrefu kutekeleza miradi kwa kisingizio cha kufanya
upembuzi yakinifu wakati fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi
zimekwishatolewa, nichukue fursa hii kuwatangazia wakandarasi wote
nchini kuanza kazi mara moja,” alisema Mgalu
Aliendelea kusema kuwa mkandarasi
yeyote atakayefanya kazi kwa kiwango kisichoridhisha atanyang’anywa kazi
na kupewa mkandarasi mwingine mwenye uwezo wa kufanya kazi kulingana na
kasi inayotakiwa na Serikali.
Alisema kuwa wananchi wengi kwa
sasa hususan walipo katika maeneo ya vijijini wanahitaji nishati ya
umeme kwa gharama nafuu, hivyo wamechoka na masuala ya michakato.
Katika hatua nyingine, Naibu
Waziri Mgalu aliwataka wakandarasi wote nchini kununua vifaa kutoka
ndani ya nchi hususan transfoma na nguzo badala ya kuagiza kutoka nje
ya nchi kama ilivyoagizwa awali.
Akielezea mikakati ya serikali
katika uboreshaji wa upatikanaji wa umeme wa uhakika na kwa gharama
nafuu, Mgalu alisema kuwa serikali kupitia REA Awamu ya Tatu inasambaza
umeme katika vijiji vyote nchini ambapo ifikapo mwaka 2019 karibia
vijiji vote vitakuwa na umeme wa uhakika.
Aliendelea kuelezea mikakati
mingine kuwa ni pamoja na matumizi ya nishati jadidifu kama vile jua
hususan katika maeneo yasiyofikiwa na umeme kutoka Gridi ya Taifa,
ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya
Mto Rufiji wa Stieglers Gorge na mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia
gesi asilia wa Kinyerezi I na Kinyerezi II.
Alisisitiza kuwa serikali imeweka
mkakati wa kufufua mkoa wa Tanga kiuchumi hivyo kuwataka wawekezaji
ndani ya nchi kuwekeza kwenye viwanda katika mkoa huo.
Alieleza kuwa kutokana na uwepo wa
mradi mkubwa wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki kutoka Hoima
nchini Uganda hadi Tanga nchini Tanzania katika mkoa wa Tanga,
mahitaji ya umeme yatakuwa makubwa hivyo Wizara ya Nishati imejipanga
katika kuhakikisha kuwa nishati ya uhakika inapatikana.
Wakati huo huo Naibu Waziri Mgalu
aliwataka wananchi wa Tanga kutoharibu vyanzo vya maji katika Bonde la
Mto Pangani yanayotumiwa katika uzalishaji wa umeme katika kituo cha
kufua umeme cha Hale ili kutoathiri uzalishaji wa umeme katika mkoa huo.
Alisisitiza kuwa serikali haitasita kuwachukulia hatua hali za kisheria wananchi watakaobainika wanaharibu mazingira.
No comments:
Post a Comment