MCHUNGAJI na waumini wa Kanisa la The
Evangelistic Assemblies of God (EAGT) mtaa wa Eden 'A' Manispaa ya
Sumbawanga, Rukwa, wamekesha wakimuombea marehemu wao afufuke, wakidai
alikufa kwa nguvu ya giza.
Elizabeth Lwitiko (30) alifariki dunia
juzi saa tatu asubuhi kutokana na matatizo ya uzazi, wakati akijifungua
pacha, aliowaacha hai na wametafutiwa mlezi.
Mchungaji Jacob Lwitiko aliongoza
waumini wake, kuchukua mwili wa marehemu chumba cha kuhifadhi maiti cha
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa, Sumbawanga na kuiweka kwenye
madhabahu ya kanisa hilo na kufanya maombezi, wakiamini kuwa huenda
atafufuka.
Mchungaji Lwitiko ni kaka wa Elizabeth
na aliachiwa uongozi wa kanisa hilo na kaka yake, Amos Lwitiko,
mwanzilishi na kwa sasa yuko Makambako mkoani Njombe. Mwenyekiti wa Mtaa
wa Edeni “A” lililopo kanisa hilo, Gerald Mwazembe alikiri kuwepo kwa
mkasa huo, uliowashitua wakazi wa jirani kwani ni mara ya kwanza
kutokea.
Akisimulia, alisema kuwa Elizabeth
alifariki dunia saa tatu asubuhi katika Kituo cha Afya cha Mazwi mjini
hapa kutokana na matatizo ya uzazi, ambapo alipungukiwa damu mwilini
baada ya kujifungua salama kwa njia ya kawaida watoto pacha ambao wako
hai.
“Mwili wa marehemu ulihifadhiwa chumba
cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa, lakini
waombolezaji na mchungaji wa kanisa hilo waliuchukua mwili huo wakiamini
alikufa kishirikina na kwamba wakimwombea angeweza kufufuka,” alieleza.
Alisema mwili ulipofikishwa kanisani
hapo, uliwekwa madhabahuni na ibada ya maombezi iliyoambatana na nyimbo
na midundo ya ngoma, ilifanyika kuanzia saa sita mchana hadi usiku wa
manane huku milango ikiwa imefungwa, wakiamini kuwa atafufuka.
“Ilipofika usiku wa manane niliwapigia
simu Polisi ambapo askari wa kikosi cha doria walifika kanisani hapo,
baada ya mazungumzo marefu waliagiza mwili wa marehemu urejeshwe na
kuhifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti ili usiharibike,”
alieleza.
Aliongeza Polisi walishuhudia mwili wa marehemu ukiwa umewekwa madhabahuni ;huku waumini wakiupapasa, wakiomba afufuke.
Baadhi ya waumini wa kanisa hilo,
walisema Mchungaji Lwitiko aliwaongoza kwa mara nyingine kuurejesha
mwili wa marehemu ili uhifadhiwe chumba cha kuhifadhi maiti cha
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa mjini hapa huku wakisisitiza kuwa
maombezi yaliyofanyika kanisani hapo ni ya imani yao.
Majirani walieleza umati mkubwa
ulifurika katika uwanja wa kanisa hilo, baada ya taarifa kuzagaa kuna
marehemu anaombewa mwili wake ukiwa madhabahuni, wakiamini atafufuka.
“Lakini walioruhusiwa kuingia kanisani
kwa maombezi, lazima awe muumini wa kanisa hilo na baada ya kuingia
mlango wa kanisa ulikuwa ukifungwa, “ alieleza mmoja wa waumini.
Mwandishi wa habari hizi alifika kanisani hapo jana asubuhi na kukuta
milango imefungwa ;huku nyimbo zikiendelea kuimbwa kanisani.
Baadaye aliambatana na Mwenyekiti
Mwazembe na mwandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten kuingia
kanisani kwa mahojiano na mchungaji, lakini ndugu wa marehemu nusura
wawapige, wakidai hawakukaribishwa msibani.
“Kwanza nyie nani... mmekuja kufanya
nini hapa ...ondokeni mara moja ....vinginevyo nendeni hospitali
mkaulize uzembe walioufanya na kusababisha kifo chake,” alifoka mmoja wa
wanandugu akitishia kuwapiga.
Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga ambaye ni
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Dk Halfany Haule
alisema anafuatilia tukio hilo na atatoa taarifa baadaye.
Taarifa kutoka kanisani hapo, zilieleza msiba huo upo Kitongoji cha Bangwe mjini Sumbawanga.
No comments:
Post a Comment