Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umeanza ukarabati wa mabweni ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) yenye ufa.
Taarifa za kuwepo nyufa hizo zilisambaa
kwenye mitandao ya kijamii usiku wa Desemba 3,2017 na baadaye ufafanuzi
ulitolewa na TBA.
Uchunguzi uliofanywa na MCL Digital
umebaini ukarabati umeanza, huku ikielezwa kuwa hauwaathiri wanafunzi
wanaotumia mabweni hayo.
“Ukarabati umeanza, mafundi wanafanya
kazi nje ya jengo kwa kuondoa plasta ili kuangalia tatizo liko wapi,”
kimesema chanzo cha habari kilichozungumza na MCL Digital.
TBA iliyojenga majengo hayo ambayo bado yako katika usimamizi wake imeelezwa pia inaangalia dosari nyingine zilizopo.
Mtendaji Mkuu wa TBA, Mhandisi Elius
Mwakalinga Desemba 4,2017 akizungumzia nyufa zilizoko kwenye jengo la
Block A alisema hazina madhara na walizitarajia.
Alisema nyufa katika jengo hilo la
hosteli ambalo ni kati ya sita yaliyopo Block A zimetokea eneo
walilotarajia ambalo kitaalamu linajulikana (expansion joint) hivyo
hazina madhara.
Mwakalinga alisema kwa kawaida udongo
unaobeba jengo hutitia baada ya muda fulani, hivyo wakati wa ujenzi
huacha nafasi kuliwezesha jengo kupumua bila kusababisha nyufa.
Mwakalinga alisema kuna makosa
yalifanyika ya kuziba nafasi zilizoachwa (expansion joint) kwa kutumia
saruji badala ya mbao au plastiki maalumu hivyo kuonyesha nyufa kwenye
jengo hilo.
Kutokana na kusambaa kwa picha kuonyesha
nyufa katika majengo hayo, mbunge wa serikali ya wanafunzi ya Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso), Kumbusho Dawson alishikiliwa na polisi
kitengo cha makosa ya mtandao kwa kuhojiwa na baadaye aliachiwa.
No comments:
Post a Comment