Mkuu wa wilaya ya Mbulu mkoani Manyara,
Chelestino Mofuga amemtaka mkazi wa kijiji cha Tumati, Faustina Boay
ambaye kwa miaka 27 alitengwa na wananchi wa eneo hilo kwa imani za
kishirikina kuwaomba msamaha ili waishi kwa amani.
Kutokana na kutengwa na wananchi hao,
Boay alipata msiba wa kufiwa na watoto wake wawili lakini alilazimika
kushirikiana na mkewe kuwazika baada ya jamii ya eneo hilo kumtenga.
Akizungumza juzi kwenye mkutano na
wananchi wa eneo hilo, Mofuga alimtaka Boay kuomba radhi kwa jamii ili
kuendelea kuishi kindugu kama miaka iliyopita.
Alisema si jambo zuri kwa Mtanzania wa
leo kujitenga peke yake na kufanya shughuli za kijamii ikiwamo kuzika
watoto wake bila kusaidiwa na wananchi wanaomzunguka ikiwamo majirani
zake.
“Nimemshauri aombe radhi kwa wananchi
ili aishi maisha kama zamani na jamii imsamehe isimtenge tena, haya
mambo ya kumuona yeye ni mpenda ushirikina yakome na kugombea mpaka wa
eneo na jirani zake uishe sasa,” alisema Mofuga.
Alisema kama ni adhabu kwa mwananchi
huyo imetosha na ameadhibiwa kwa muda mrefu kwa kuwa miaka 27 aliyoishi
yeye na familia yake bila kushiriki shughuli za kijamii inatosha
kumfanya ajirudi na kufungua ukurasa mpya wa maisha na wananchi wenzake.
Hata hivyo, Mofuga alipinga vikali
kitendo cha wananchi wa kijiji hicho kuchoma nyumba ya Boay kwa kile
kinachodaiwa kuwa ni kulipiza kisasi wakimtuhumu kufanya ushirikina kwa
kumloga jirani yake.
“Suala la kuchoma nyumba ya Boay
siliungi mkono hata kidogo kwani huko ni kujichukulia sheria mkononi na
ninawapongeza askari polisi waliowakamata wahusika wa tukio hilo,”
alisema Mofuga.
Kwa upande wake, Boay ambaye kwa zaidi
ya miaka 27 alikuwa amejitenga na jamii hiyo ikiwamo kutohudhuria
sherehe au misiba inayotokea kijijini hapo, alisema ataufanyia kazi
ushauri huo.
“Hata mimi nimechoshwa na maisha haya
kwani jamii ilitutenga na kutuacha wenyewe mimi na familia yangu pekee,
hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kutekeleza maagizo ya mheshimiwa mkuu wa
wilaya,” alisema Boay.
No comments:
Post a Comment