Mwanamuziki Wilson Abubakar Radido almaarufu Willy Paul alikutana na naibu wa Rais katika jamhuri ya Kenya Mheshimiwa William Samoei Ruto katika makazi yake ya Karen.
Naibu wa Rais aliweka picha kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii akionekana kucheka na kufurahi na mwanamuziki huyo wa kizazi kipya.
Alielezea kwamba anawekeza kwa vijana kupitia sanaa kama vile muziki, densi, michezo ya kuigiza na nyingine ili kuinua mabadiliko chanya katika uchumi na jamii kwa ujumla.
Alielezea pia kwamba wamekubaliana kushirikiana na Willy Paul anayefahamika sana kwa wimbo wake “sitolia” ili kuhakikisha kwamba uchumi wa sekta ya burudani unakua.
Willy Paul kwa upande wake hakutoa maelezo kuhusu mkutano huo na naibu wa Rais ila aliweka picha na kuongeza #Colabo #Ruto kuashiria ushirikiano kati yao.
Naibu wa Rais ameonyesha nia ya kuwania Urais wa nchi ya Kenya kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 na amekuwa akikutana na watu wa tabaka mbali mbali anapopanga mikakati yake.
Jumatatu Naibu wa Rais alihudhuria hafla ya uzinduzi rasmi wa ripoti iliyorekebishwa ya BBI, jumanne akakutana na baraza la wazee nchini Kenya na jana Jumatano ilikuwa zamu ya Willy Paul.
Inasubiriwa kuona jinsi ushirikiano huo wao utatekelezwa.
No comments:
Post a Comment