Baba Mtakatifu Francisko amekubali ombi
lililowasilishwa kwake na Askofu mkuu Josephat Louis Lebulu wa Jimbo kuu
la Arusha, Tanzania la kung’atuka kutoka madarakani.
Wakati huo huo, Baba Mtakatifu amemteua
Askofu Isaac Amani Massawe wa Jimbo Katoliki Moshi, kuwa Askofu mkuu
mpya wa Jimbo Kuu la Arusha, Tanzania.
Askofu mkuu mteule Isaac Amani Massawe, alizaliwa tarehe 10 Juni 1951 huko Mango, Jimbo Katoliki la Moshi.
Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, akapadrishwa kunako tarehe 29 Juni 1975.
Tarehe 21 Novemba 2007 akateuliwa na
Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Moshi
na kuwekwa wakfu tarehe 22 Februari 2008 na Kardinali Polycarp Pengo,
Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam akisaidiana na Askofu mkuu
Josephat Louis Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha pamoja na Hayati Askofu
Amedeus Msarikie wa Jimbo Katoliki la Moshi.
Hivi karibuni, aliteuliwa pia kuwa ni Msimamizi wa Kitume Jimbo Katoliki la Mbulu.
Kwa ufupi, Askofu mkuu mteule Isaac
Amani Massawe alisoma shule ya msingi Mango, Kibosho; Seminari ndogo ya
St. James, Moshi; Falsafa kati ya mwaka 1970 – 1972, Seminari kuu ya
Ntungamo, Jimbo Katoliki Bukoba.
Alijipatia masomo ya Taalimungu Seminari
kuu ya Kipalapala, Jimbo kuu la Tabora kati ya mwaka 1972 – 1975 na
hatimaye, kupadrishwa mwezi Juni 1975. Kama Padre aliwahi kuwa Paroko
usu, mwalimu na mlezi wa Seminari ndogo ya St. James, Moshi.
Kati ya Mwaka 1986 hadi mwaka 1989
alikuwa masomoni, Chuo kikuu cha Walsh, nchini Marekani; kati ya mwaka
1990 hadi mwaka 2003, mlezi wa watawa na baadaye akateuliwa kuwa ni
Paroko wa Kanisa kuu la Kristo Mfalme, Jimbo Katoliki la Moshi.
No comments:
Post a Comment