Bodi
ya Wadhamini ya Kanisa la Evangelistic Assemblies Of God Tanzania
(EAGT) imemsimamisha Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Mchungaji Brown
Mwakipesile ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili.
Wengine waliosimamishwa leo Desemba 18 ni Katibu Mkuu, Mchungaji Leonard Mwizarubi na Mhasibu Mkuu, Mchungaji PrayGod Mngonja.
Pamoja na mabadiliko hayo, bodi imewateua kwa muda kushika nafasi hizo,
Askofu Mkuu atakuwa ni Mchungaji Asumwisye Mwaisabila, Katibu Mkuu
atakuwa Dk Jakob Madaha na Mhasibu Mkuu atakuwa Andrea Salu.
Kwa mujibu wa Katiba ya EAGT ya Mwaka 2011 ,ibara ya 6(b)(5) kinatoa
mamlaka Kwa Wajumbe wanne wa bodi hiyo kusimamisha viongozi wakuu wa
kanisa akiwamo Askofu Mkuu kabla ya Mkutano Mkuu kujadili maazimio hayo.
"Baada ya siku 30 kuanzia leo tutakuwa na mkutano mkuu wa Kanisa kwa
ajili ya kupitisha mabadiliko hayo, wamesimamishwa kwa kumfukuza Makamu
Askofu Mkuu wakidai alitenda dhambi, walimfukuza uchungaji na uumini
pia," ni kauli ya Mwenyekiti wa bodi hiyo, John Mfuko alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari.
Mzee Mfuko ambaye anazungumza kwa taabu kutokana na umri wake alisema
kosa la viongozi hao wa kanisa ni kumfukuza bila kushirikisha bodi ya
Wadhamini.
Mzee Mfuko aliyeongozana na wajumbe wawili kati ya wanne wa bodi hiyo
alisema licha ya mahakama kubatilisha suala la kumfukuza, Askofu Mkuu
(aliyefukuzwa) alikataa kumrejesha kanisani. Tuhuma nyingine ni
kushiriki njama za kuhujumu mali za kanisa.
Baada ya kutafutwa kwa simu yake ya mkononi, Askofu aliyesimamishwa Mwakipesile hakupatikana kwenye simu yake ya mkononi.
Mbali na tuhuma hizo, bodi imewataka waumini wa kanisa hilo kutotuma
pesa katika akaunti za kanisa huku ikiweka wazi kushikilia akaunti hizo
kutoka mikononi mwa viongozi waliokuwa na dhamana ili kuhakiki wa mali
za kanisa.
No comments:
Post a Comment