Kibaha. Vijana 12 mmoja wao akiwa ni msichana wanaodhaniwa ni wezi wamevamia kwenye nyumba ya watawa wa Shirika la Botania kutoka nchini India na kuwajeruhi kisha kupora vitu mbalimbali.
Kundi hilo pia lilivamia eneo la kanisa wanalolitumia kusali na kuiba vifaa maalumu vya kufanyia ibada ikiwemo tabenako na ekaristi takatifu na kikombe kiitwacho ciborium wakiondoka navyo.
Tukio hilo lilitokea saa 7:00 usiku wa kuamkia leo katika kijiji cha Vikuge Kibaha, mkoani Pwani ambapo vijana hao mbali na kupora vitu hivyo wanadaiwa kumjeruhi mmoja wa watawa hao sehemu za usoni kwa kutumia kitu chenye ncha kali.
Kamanda wa Polisi Mkoani Pwani Wankyo Nyigeza alipoulizwa kuhusu tukio hilo alisema ana taarifa zake lakini hayupo tayari kulielezea wakati huo.
"Ni kweli hilo tukio tunalo lakini mbona nilishasema sipo tayari kulizungumzia kwa sasa," alisema Wankyo.
Akizungumza na Mwananchi Paroko wa Parokia ya Mt.Don Bosco Kibaha mkoani Pwani Padri Beno Kikudo alisema vijana hao walipofika kwenye makazi ya masista hao walivunja milango kisha kuingia ndani na kutekeleza uhalifu huo kisha kutokomea kusikojulikana.
Kikudo alisema tukio hilo ni sawa na najisi kwa kitu cha ibada kulingana na imani ya dhehebu la kikatoliki kwani matukio mengine ya kuiba fedha na vitu vingine ni kitu cha kawaida.
"Lakini wanapokuja kwenye kitovu cha imani ya kanisa sio kitu kizuri kwa upande mmoja ni kuwaombea labda hawajui kinachofanyika lakini kubwa ni kuona kabisa kuwa ulikuwa ni wizi ambao siyo ulikuwa tu wa kujeruhi na kuiba lakini kibaya kuiba vitu vya kanisa," aliongeza.
Padri Kikudo alishauri suala la ulinzi shirikishi liendelee kutekelezwa na kuomba wananchi wenye nia njema kutoa taarifa pindi wanapoona uwepo wa watu wasio wa kawaida siyo kwa tukio hilo tu bali kwa lolote kwenye maeneo hayo.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Hospitail ya rufaa ya Mkoa wa Pwani Dk Edward Wayi amethibitisha kuwapokea watawa hao watatu wawili wakiwa ni raia kutoka nje ya nchini wakiwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili.
Alisema waliwafanyia vipimo na kuwatibu lakini bado wanaendelea kuwafanyia uchunguzi na kuendelea kuwapatia matibabu wakitoka nyumbani kwao.
"Ni kweli tuliwapokea watawa watatu waliodai kuumizwa maeneo mbalimbali ya mwili na watu wasiojulikana sasa yaliyotokea huko mimi siyo rahisi nieleze ila sisi tuliwafanyia uchunguzi, vipimo na kuwatibu kisha tuliwaruhusu kuondoka na kwamba bado tunaendelea kuwafanyia uchunguzi na matibabu wakitokea nyumbani,” aliongeza Dk Wayi.
No comments:
Post a Comment