By Pamela Chilongola
Dar es Salaam.
Mwimbaji wa nyimbo za injili, Rebecca Magaba amesema aligundua aliyekuwa mumewe, Zabron Maselege hana korodani usiku wa siku waliyofunga ndoa.
“Sisi ni walokole, unapochumbiwa na mwanamume huruhusiwi kukutana naye hadi siku unapofunga ndoa. Baada ya kufunga ndoa na mume wangu matatizo ndipo yalipoanza,” alisema Rebecca mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Buruguni, Mwinyiheri Kondo.
Hata hivyo, Mahakama hiyo ilivunja ndoa ya mwimbaji huyo baada ya wanandoa hao kutoshiriki tendo la ndoa kwa miaka 18.
Akitoa ushahidi mahakamani, Rebecca alisema alikutana na mume wake kwenye makambi na ndipo urafiki wao ulipoanza.
Rebecca, aliyetamba na wimbo wake wa ‘Ebenezer’ alikuwa anasali katika makanisa ya kilokole.
Alisema baadaye Maselege aliyekuwa akiuza urembo wa kutembeza jijini Mwanza, alikuwa anafika kwenye duka lake mara kwa mara na kumweleza kuwa anataka aende nyumbani kwa wazazi wake ili amchumbie.
Rebecca alisema kwa kuwa alikuwa anampenda alimkubalia na akaenda kumtambulisha kwao na alikubaliwa kulipa mahari ya Sh200,000 lakini alitoa Sh100,000 tu.
Alisema mipango ya harusi ilifanyika, lakini kwa kuwa upande wa mume wake haukuwa vizuri kimaisha, alilazimika kugharamia harusi hiyo, hivyo Maselege alitoa fedha kwa ajili ya kushona tu suti yake.
Rebecca alisema mwaka 2002 walifunga ndoa ya Kikristo mkoani Mwanza, lakini kabla ya ndoa hiyo walikuwa wanaishi vizuri hawakuwahi kugombana wakati wa uchumba wao.
Rebecca alisema baada ya kufunga ndoa na mume wake, walirudi nyumbani huku akiamini siku hiyo ndiyo furaha yake ya kukutana na mumewe lakini ilikuwa tofauti na matarajio yake.
Alidai walipoingia chumbani alitegemea wangefanya tendo la ndoa, matokeo yake mume wake alilala na kugeukia upande wa pili huku akidai amechoka kutokana na pilikapilika za sherehe amvumilie yeye ameshakuwa mume wake.
Rebecca alisema alimsikiliza, wakalala lakini mambo yaliendelea vivyo hivyo, hadi kufikia siku ya tano ndipo alimfuata rafiki wa Maselege na kumweleza yaliyokuwa yakimsibu.
Alisema baadaye alilazimika kwenda kanisani kumweleza mchungaji aliyewafungisha ndoa hiyo, mume wake aliitwa na kuelezwa lakini aliwaeleza hana shida ilikuwa ni uchovu mambo hayo wataenda kuyamaliza.
Rebecca alisema walirudi kutoka kanisani na walipoingia chumbani mume wake alimweleza anataka kumwambia kitu lakini asimwambie mtu yeyote amfichie siri, ndipo alipanda kitandani na kumuonyesha sehemu zake za siri huku akimweleza hana korodani zote mbili na hajawahi kutoa mbegu za kiume na hana nguvu za kiume.
Rebecca alidai baada ya kuelezwa hayo alimuuliza mume wake kwa nini asingemwambia kabla ya kufunga ndoa, lakini alimjibu angemweleza hayo wasingekuwa wote.
Alisema mbela ya hakimu kuwa, baada ya kuelezwa hayo alichanganyikiwa, ndipo alikwenda kutoa taarifa kwa mchungaji wa kanisa lao, lakini alimwambia huyo ni mume wake wameshafunga ndoa kinachotakiwa waendelee kufanya maombi pamoja na matibabu.
Rebecca alisema baada ya kuelezwa hayo, walirudi nyumbani ndipo mume wake alimweleza ameamua kwenda kumdhalilisha kwa wachungaji wakati walishaelewana amfichie siri hiyo ndipo alianza kumpiga.
Baada ya kuelezwa hayo, Rebecca alisema alimvumilia mume wake na waliishi kwa zaidi ya miaka 18 ya ndoa yao huku mume wake akifanyiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza ya Sekou Toure.
Rebecca alidai wakati mume wake anaendelea na matibabu katika hospitali hiyo, ndipo daktari aliyekuwa anamtibu alimweleza kama anampenda mume wake akazae na kaka yake kwa kuwa majibu yaliyotoka yanaonyesha hana uwezo wa kumpa mimba.
“Tuliporudi nyumbani mume wangu aliniuliza; wachungaji wamekutuma uje unidhalilishe? Ndipo akachana vyeti vyote tulivyotoka navyo hospitalini na kuanza kunipiga huku akinisukuma; niliangukia kwenye stuli ya kioo na kunikata,” alisema Rebecca.
Akiendelea na ushahidi mahakamani hapo, alisema wakiwa ndani ya mwezi mmoja tangu wafunge ndoa, mume wake alimchoma usoni na kwenye paja lake kwa kutumia pasi ya umeme.
“Mume wangu alivyoona kila mtu ameijua tabia yake, ndipo mwaka 2015 aliniambia tuhamie Dar es Salaam kutoka Mwanza. Tuliishi eneo la Segerea, lakini tabia yake ya kupiga iliendelea ndipo mwaka 2017 nilitengana naye rasmi,” alisema Rebecca.
Akitoa ushahidi mahakamani hapo, Rebecca alisema baada ya kutengana na mume wake aliitwa na wachungaji pamoja na maaskofu na kuulizwa kwanini wametengana na kuwaeleza kuwa amemvumilia kwa tatizo lake hilo, lakini ameshindwa kuvumilia kupigwa.
Baada ya askofu kushindwa kuwasuluhisha, alimweleza aende mahakamani.
“Hadi sasa ni miaka minne tumetengana; kilichonifanya niondoke kwa mume wangu alikuwa ananifanyia vitendo vya unyanyasaji nisije nikafa bure, kwa dhehebu letu ukiolewa umeolewa huwezi kuachana na sikuwahi kumnyanyapaa upigaji ndio umenifanya tuachane,” alisema Rebecca.
Akitoa hukumu, Hakimu Kondo alisema Mahakama hiyo imevunja ndoa ya Rebecca na Maselege, hivyo mali zote walizochuma wanandoa hao ikiwamo shamba la eka 10 lililopo Bagamoyo (Pwani), maduka mawili yaliyopo Bonyokwa (Dar es Salaam), majengo na shamba la miti ya mikalatusi eka moja lililopo mkoani Kigoma zichukuliwe na Maselege na kiwanja kilichopo Madale (Dar es Salaam) kitabaki kwa Rebecca.
Hakimu Kondo alisema amevunja ndoa hiyo baada ya kuona wanandoa hao wanafanya matendo ya ndoa ambayo si ya kawaida.
Hata hivyo, alitoa siku 45 ya kukata rufaa kwa mdaiwa.
No comments:
Post a Comment