Maofisa wa polisi katika Kaunti ya Kirinyaga wanawashikilia
wanandoa Mary Wambui na mumewe Joseph Maina ambao ni wazee wa kanisa kwa
madai ya kuiba mali za kanisa zenye thamani ya Sh300,000.
Wawili hao ambao ni washirika wa kanisa la Seventh Day Adventist
(SDA) tawi la Kang’aru walipanga njama ya wizi na kufanikiwa kuiba mali
hizo na kuficha nyumbani kwao wakingojea kutafuta soko.
Kwa mujibu wa Mkuu wa polisi wa eneo hilo, Hillary Mwaniki amesema
kwamba wanandoa hao walitekeleza wizi huo usiku wa kuamkia leo Jumatatu.
Wanandoa hao wanadaiwa kuiba viti 64, kompyuta 1 na vipaza sauti 3, mali ambazo zilikutwa zimefichwa nyumbani kwao.
“Inaaminika kuwa wawili hao walishirikiana na mwanamume mwingine
ambaye kwa sasa yupo mafichoni walitekeleza wizi huo usiku wa manane
baada ya kuvunja mlango wa kanisa. Aidha, tunachunguza kama watatu hao
ndio waliibia makanisa mengine mawili katika eneo hilo usiku huohuo,”
akasema.
Bw Mwaniki aliarifu kuwa majirani wa washukiwa hao ndio walitoa taarifa polisi na kisha kutiwa mbaroni.
“Tunawashukuru raia kwani wao ndio waligundua wezi hao na pia
wakawasiliana na maafisa wetu wa polisi ambao waliwasili na kupata
washukiwa hao tayari walikuwa wametiwa mbaroni na wenyeji. Ushirikiano
huo ulizuilia mali hiyo kuuzwa kabla ya ugunduliwe,” akasema.
Bw Mwaniki alisema kuwa washukiwa hao watafikishwa mahakamani ili
wajibu mashtaka ya kuiba mali ya kanisa huku harakati za kumsaka
aliyekimbia zikiendelea kufanywa na polisi.
No comments:
Post a Comment