Mtendaji wa Kata ya Mwandui iliyopo
mwambao wa bonde la ziwa Rukwa, wilayani Sumbawanga mkoani hapa,
Benedict Chapewa ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando amesema tukio hilo limetokea usiku
wa kuamkia leo, Mei 2,2018.
Kamanda Kyando amesema Chapewa ambaye
amewahi kuwa Katibu Mwenezi, CCM Wilaya ya Sumbawanga, alivamiwa na
kundi la watu wasiojulikana wakati akiwa anakunywa pombe katika moja ya
baa anayomiliki kijijini hapo.
“Watu hao walimmiminia risasi kwa
kutumia bunduki aina ya gobore kisha kumkata kata na mapanga sehemu
mbalimbali za mwili wake,” amesema.
Amesema baada ya wauaji kutekeleza
adhima yao waliondoka kuelekea kusikojulikana na hawakuchukua kitu
chochote kutoka kwa marehemu au katika baa hiyo.
Kamanda Kyando amesema uchunguzi wa kina
kuhusu tukio hilo unaendelea kufanyika na watuhumiwa wanasakwa popote
walipo ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo
kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi kwani kufanya hivyo ni
ukiukaji wa haki za binadamu na vyombo vya dola vitahakikisha
vinawachukulia hatua za kisheria wale wote wanajichukulia sheria
mkononi.
No comments:
Post a Comment