Katika kutekeleza sera ya Tanzania ya viwanda takribani akina mama 2000
mkoani Kigoma wanatarajia kupata mafunzo ya ujasiriamali yatakayosaidia
kuwaimarisha kiuchumi.
Awali akifungua rasmi mafunzo hayo ambayo leo mkoani humo yanatarajiwa
kudumu kwa muda wa siku 10 katika halmashauri zote mkoani Kigoma Katibu
Tawala msaidizi wa Mkoa wa Kigoma Gaden Machunda aliwataka akina mama
hao kuwa makini kusikiliza mafunzo watakayopata ili kuleta maendeleo ya
mkoa na taifa kwa ujumla
Aliwasisitiza akina mama kujikita katika ujenzi wa viwanda kuelekea uchumi wa kati ifikapo 2028.
Aidha Machunda aliwataka akina mama kuzingatia misingi ya ujasiriamali
pamoja na kuwa na nidhamu na biashara wanazozifanya huku akiwataka
wauzaji wa hoteli pamoja na migahawa kuwa nadhifu ili kuwavutia wateja.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Kampuni ya AJ General Company
alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha wanawake pamoja na kusaidia
kutekeleza ilani ya serikali ya awamu ya 5 kuelekea ujenzi wa Tanzania
ya viwanda.
Alisema kupitia mpango huo wanawake wataweza kuinuka kiuchumi na kupata
mikopo isiyokuwa na masharti kama ilivyokuwa hapo awali lakini pia
kuwezesha bidhaa zinazozalishwa mkoani Kigoma kupata soko nje ya nchi.
Katibu wa Umoja wa wanawake (UWT) mkoani Kigoma ,Edina Kuguru alisema
wao kama viongozi wa wanawake wamejipanga kuhakikisha wanawake wote
mkoani humo wanaondokana mfumo wa kuwategemea wanaume kwa kuanzisha
warsha na semina mbali mbali za ujasiriamali.
Alisema mikakati waliyonayo ni kutoa elimu ya ujasiriamali na jinsi ya
kutumia fedha wanazopewa zinatumika ipasavyo na kuwatafutia masoko kwa
kuwa wana mipango ya kuanzisha viwanda vya mihogo na kwa kuwa zao hilo
linalimwa sana mkoani Kigoma na ni rahisi kulifanyia uwekezaji.
Hata hivyo alisema Mafunzo ya ujasiRiamali na uwezeshaji kwa wanawake
yameanza kufanyika mkoa wa Kigoma kwa kuwa ni mkoa ulioshinda kati ya
mikoa mitano iliyopeleka mapendekezo yake na wanaohitaji mafunzo hayo na
kukawa na zaidi ya wanawake 2000 waliojiandikisha kushiriki mafunzo
hayo.
Mmoja kati ya wanawake wajasiriamali Mkoani Kigoma, Maisala Barakabise
alisema wanawake wa Kigoma wanajitahidi kufanya biashara kwa kutumia
mitaji yao na wao ndiyo walezi wa familia na ni wathubutu wakiwezeshwa
wanaweza zaidi wao wanashughulika na fursa nyingi mkoani Kigoma
zinaibuliwa na wanawake na kuzifanyia kazi.
Alisema changamoto wanazokumbana nazo katika kutafuta kipato na
kujiondoa katika dimbwi la umasikini ni kuwa na mitaji midogo na hili
linasababisha watoto wanapokwenda vyuoni wazazi wanalazimika kuchukua
mitaji waliyonayo kuwalipia ada watoto wao waweze kusoma kwa kuwa
asilimia kubwa ya Wanawake mkoani Kigoma wanalea familia peke yao.
Kwa upande wake Sakina Kabeza mjasiriamali alisema wanawake wa Kigoma ni
wachapakazi na wanajituma kipindi cha nyuma fursa zilikuwa ni chache
lakini kwa sasa awamu ya tano imejipanga kikamilifu kutoa fursa kwa
wanawake wote na endapo wanawake wa Kigoma wakipatiwa elimu na mitaji
wana uwezo wa kufanya vitu vya tofauti sana na kuwaasa wanawake wengine
kuchangamkia fursa zilizopo ili kujikwamua na maisha duni.
Aidha aliipongeza taasisi hiyo iliyojitokeza na kutoa elimu na mikopo
kwa wanawake mkoani Kigoma na kwamba wanawake wa Kigoma
wanajishughulisha na biashara mbalimbali endapo watapatiwa mikopo hiyo
itasaidia kuinua uchumi wao na kuanzisha viwanda vya Mihogo na Samaki
kwa kuwa ni mazao ambayo wanawake wengi wanajishughulisha nayo fedha
hizo zitasaidia kuboresha mitaji na biashara zao.
No comments:
Post a Comment